HOMA ya ini ni ugonjwa unaoelezewa kuwa ni kuvimba kwa ini. Ini ni kiungo katika mwili wa binadamu kinachofanya kazi muhimu sana kama kuchuja, kupambana na hata kuondoa sumu mwilini.
Kuna vitu vingi vinavyoweza kusababisha homa ya ini lakini katika makala hii tutaongelea kuhusu homa ya ini inayosababishwa na virusi vya homa ya ini kama vinavyojulikana au kuitwa.
Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo, umekuwapo kwa miaka mingi lakini uelewa umekuwa mdogo na hafifu juu ya ugonjwa huu.
Hali hii inahusishwa na watu kutokuelewa ni nini hasa maana ya ugonjwa huu. Watu waliosoma pia wamekuwa na uelewa hafifu juu ya janga hili na wamefanana na wale ambao hawakupata bahati ya kupata mwanga wa kujua mambo ya kidunia- wasiokwenda shule.
Kwa sasa katika hospitali, vituo vya afya na makongamano ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, ikiwemo Siku ya Homa ya Ini Duniani, Julai 28 kila mwaka, watu wamekuwa wakiamshwa kuhusu uelewa wa ugonjwa huu. Watu wametafuta kujua hali zao mapema na hata kupata matibabu pale inapotakiwa.
AINA ZA HOMA YA INI
Kuna aina tano za Homa ya Ini ambazo zimepewa majina yao kutokana na herufi za alifabeti, yaani aina A,B,C,D,E.
Aina ya kwanza ya Homa ya Ini, yaani aina A, imeonekana kuambukizwa kwa njia ya chakula na mdomo, ikimaanisha kumpata mtu pale anapokula chakula kichafu kisicho safi na salama, chenye maambukizi ya virusi hivi vya homa ya ini. Pia kunywa maji au chakula kilicho na kinyesi ndani yake.
Aina hii ya virusi huambukizwa kwa urahisi na wepesi sana. Jambo zuri ni kwamba kuna chanjo yake ya kuzuia maambukizi ya virusi hivi.
Aina ya pili, yaani aina B, ni moja ya virusi vinavvyoweza kusababisha madhara makubwa sana kama saratani ya ini au kushindwa kufanya kazi kwa ini lenyewe. Virusi hivi huambukizwa kwa majimaji ya mwili kama jasho na mate, manii wakati wa kujamiana, kwa damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua au ujauzito, kuchangia vitu vya ncha kali kwa kujichoma.
Pia aina hii ina chanjo ya kuzuia maambukizi yake lakini huweza kupewa pale tu unapoweza kupima kama tayari una maambukizi tayari au la. Chanjo yake huweza kutolewa siku ya kwanza baada ya kupima na kukutwa huna maambukizi hayo, baada ya mwezi moja, mitatu au sita baadaye.
Aina ya tatu ya virusi ya Homa ya Ini (aina C) hufanana na maambukizi ya aina B kwenye maambukizi na hata madhara ya baadae. Tofauti yake ni kwamba yenyewe haijapata chanjo yake mpaka sasa lakini ina matibabu yake. Matibabu yake huweza kuchukua wiki nane mpaka 12 kwa kutumia dawa za kutibu aina hii.
Aina ya nne ya Homa ya Ini (aina D), ni moja ya virusi visivyokuwa na chanjo mpaka sasa. Jambo zuri ni kwamba huwezi kuipata kama huna tayari maambukizi ya aina ya B, hivyo kama umepata chanjo ya kuzuia Homa ya Ini ya aina ya B, huwezi kupata aina hii pia. Aina hii pia huambukizwa kama ilivyo aina B na C.
Aina ya mwisho, yaani D, maambukizi yake huwa kama aina ya kwanza ya A, yaani kunywa maji machafu au yenye maambukizi ya virusi hivi au chakula kama nyama ambayo haijapikwa ikaiva vizuri. Aina hii ni hatari pale inapompata mjamzito kwa kuwa inaweza kusababisha madhara zaidi. Pia haina chanjo lakini huweza kuzuilika kwa kujikinga.
DALILI ZA HOMA YA INI
Dalili za Homa ya Ini zimekuwa zikifanana na dalili za magonjwa mengine hiyo imesababisha kuwa changamoto ya kujua kama kweli mtu ana ugonjwa huu tayari. Jambo muhimu zaidi kufanya ni kupima ugonjwa huu kwa njia ya damu kugundua kama una tatizo hili tayari na kuanza matibabu mara moja.
Dalili zake ni pamoja na kuhisi kuumwa,viungo na misuli kupasuka, mwili kuchoka na kuisha nguvu, kichefuchefu na kutapika, mwili kupata homa, macho kuwa ya njano, mwili kuwashwa, kupata mkojo mweusi kama chai au kupata choo kisicho na rangi.
KINGA NA MATIBABU
Matibabu ya Homa ya Ini kuweza kufanyika tu pale mtu anapogundulika kuwa na tatizo hilo. Ni ngumu kwa kuangalia na kujua kama mtu ana maambukizi tayari, hivyo inampasa mtu kupima ili kujua.
Kuzuia ni pamoja na kupata chanjo kwa aina zilizo na chanjo, kuzingatia usafi wa chakula na mazingira, kuepuka kufanya ngono zembe kwa kufanya mapenzi na mtu usiyemtambua afya yake, kuepuka kuwa na wapenzi wengi ambao huweza kuleta urahisi wa maambukizi na kuacha kuchangia vitu vya ncha kali.
Uelewa wa swala hili huweza kuzuia maambukizi mapya na kuzuia madhara ya baadae yanayoweza kukumba vizazi vyako vyote vijavyo. Fuata ushauri wa daktari wako na pima afya yako sasa.
· Dk. Budodi ni daktari wa tiba ya binadamu na anapatikana jijini Dar es Salaam. Kwa ushauri unaweza kumpata kwa baruapepe [email protected] au simu namba 0710 980096
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED