Viashiria uovu nyumba ya baba yako

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 12:05 PM Feb 09 2025
Baba na wanawe
AI
Baba na wanawe

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na mada ya wiki iliyopita kuhusu uovu wa nyumba ya baba zetu unavyotesa watu wengi. Yako mambo yanakutokea leo na kukutesa, kumbe yanatokana na uovu wa baba yako uliojificha.

Nikasema kuwa uovu uliojificha unafanya ukatili mkubwa sana wa viwango vya juu kwenye maisha ya watu.   

Lakini hicho kilichojificha ni zile nguvu za laana zilizoachiliwa kwenye nyumba za baba zetu. Yamkini wewe ni shuhuda huwa unaona kila mwaka matambiko yanayofanyika kwenye nyumba ya baba yako kutia nguvu ule uovu! 

Hebu leo twende zaidi juu ya jambo hili. Mahali popote ambapo yalifanyika mambo haya yafuatayo utagundua hiyo nyumba upo uovu uliojificha. 

Kama kwenye familia yako wako watu wa aina hii na walifanya mambo haya yafuatayo, ujue upo uovu umejificha pale. Ambao kama hautashughulika nao utaendelea kuharibu maisha yako daima.

Haijalishi wewe ni nani kwani ile ni sheria inatafuta na kama hujaijua haiwezi kubadilika wala maisha hayawezi kubadilika. (Zaburi 74:20) “Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili”.

Mahali penye giza ni mahali ambapo pana dhambi halafu pana uovu umefanyika. Ni nyumba yenye kuabudu miungu ndipo mahali penye giza!

Kama kwenye nyumba au familia ya kwenu kuna watu wanaabudu miungu mpaka sasa na ifikapo kila mwezi wa 12 huenda kuitambikia, kuitolea sadaka au wana desturi ya kuabudu makaburini na kuabudu miungu hadi sasa, hapo panaitwa mahali penye giza.

Na hapo penye giza, pamejaa makao ya ukatili. Na huo ukatili ni yale mambo mabaya, maovu yanayotokea. Kama unatoka kwenye ukoo unaoabudu miungu, hiyo sehemu tayari ina giza.

Hapo giza limetanda na ukatili ndio maana vifo kila mwaka, maisha hayaendi, watu wanakutana na ukatili usio wa kawaida. Kumbe kuna mahali penye giza jambo baya lilifanyika.

Kuna watu wako mjini lakini nyumba ya baba yako kuna vitu vinaendelea. Uko hapa unapambana na maisha lakini kuna nguvu inayofanya kazi kuanzia kwenye nyumba ya baba yako, ukoo wenu.

Na hiyo nguvu inafanya kazi kutokana na kuwepo miungu iliabudiwa na wanaendelea kuitolea sadaka. Ndio maana uharibifu mkubwa utakaokutokea ni ule unaotoka kwenye nyumba ya baba yako.

Andiko  la Mungu linasema, “Kama misingi ikiharibika, mwenye hali atafanya nini? (Zab.11:3). Kadiri unavyoendelea kufanya matambiko, kuna madhara yanafuata.

Kama hautafanya jambo la kushughulika na nyumba ya baba yako, ipo nguvu ambayo itakuwa inafanya kazi katika maisha yako. Wewe utabaki unajiuliza, mbona mambo hayaendi, mbona hakuna chochote kinachotokea. Hapana, hii ni nguvu iliyojificha kwenye nyumba ya baba yako.

Kumbuka wewe una damu ya baba yako. Ndio maana ili kujua mtoto ni wa baba yupi, damu ndiyo inayopimwa kitaalamu kujua vinasaba. Kwa hiyo uovu ule ulioanzia kwenye nyumba ya baba yako, upo kwenye damu yako.  

Unakuta kuna jambo unalisukuma kulifanya na unaingia kwenye matatizo makubwa, mwisho unajuta unajiuliza ni kitu gani? Kumbe ni ule uovu unatembea kwenye damu ya baba yako. 

Mfano, kwenye maandiko ya Mungu inatajwa baraka za Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Lakini ukirudi utagundua kuna mambo yalikuwa siyo mazuri yaliyokuwa yakitembea kuanzia Ibrahimu, Isaka na Yakobo.

Pamoja na kwamba kulikuwa na mtembeo wa baraka, lakini kulikuwa na mtembeo wa uovu fulani uliokuwa unafanya kazi ukifuata damu.

Utagundua kulikuwa na roho au laana ya kudhulumiwa. Ndio maana ukishaanza kuota kwenye ndoto ni kama vile unafukuzwa, unadhulumiwa hiyo ni nguvu fulani. Unanyang’anywa vitu kwenye ndoto tayari kuna shida.

Ibrahimu alinunua kisima, Isaka alipokichimba chenyewe akanyang’anywa. Yakobo akadhulumiwa mshahara zaidi ya mara kumi wakati anafanya kazi kwa Labani. Ukigundua sintofahamu ya aina hiyo ukafanya maombi ya kukata mawasiliano utatoka kwenye kadhia hiyo. 

Bila shaka lipo jambo umejifunza hapo.  Wiki ijayo tutaendelea na viashiria zaidi vinavyotesa wengi. Kumbe chimbuko ni ule uovu uliojificha kwenye nyumba ya baba yako. Una maoni, kisa cha kimaisha? Ujumbe mfupi 0715268581. Pia namba hii ipo WhatsApp.