Majaliwa awashukia wanaong'oa mabango, nguzo anuani za makazi

By Renatha Msungu , Nipashe Jumapili
Published at 11:55 AM Feb 09 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaong’oa mabango na nguzo za anwani za makazi na kwenda kuuza.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana jijini hapa wakati wa kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi sambamba na kuzindua matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi.

Alisema ni muhimu wananchi kutunza na kuwa walinzi wa miundombini ya anwani za makazi kwenye maeneo yao kwa kuwa serikali imetumia gharama kubwa katika kugharamia uwekaji huo.

"Vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara, tunao Watanzania ambao si waaminifu wanang’oa mabago hayo na kwenda kuyauza, ni muhimu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa sababu ina manufaa," aliagiza.
 

Waziri Mkuu alisema suala la anwani za makazi ni moja ya yaliyopewa kipaumbele katika Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022- 2025/2026, ambao umeweka bayana azma ya serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi katika kata zote nchini.

"Siku kama ya leo, Rais Samia alizindua utekelezaji mfumo wa anwani za makazi nchini kwa njia ya operesheni. Operesheni hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi minne na kuwezesha ukusanyaji taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi zilizohifadhiwa katika mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi unaojulikana kwa jina la National Physical Addressing (NaPA)," alisema.
 

Alibainisha kuwa kupitia programu ya NaPA, mwananchi akiwa eneo lolote nchini na hajui sehemu ya kupata huduma za kijamii kama vile kituo cha afya au mgahawa, anaweza kutumia programu hiyo kutafuta sehemu za karibu.

"Hii ni programu bora na inarahisisha kupata huduma husika sambamba na kwenda na kasi ya kimaendeleo katika uchumi wa sasa wa kijiditali," alisisitiza.
 

Alifafanua kuwa mfumo wa anwani za makazi utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi, kuharakisha upatikanaji huduma za kijamii, kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama, kuwezesha biashara mtandao kufanyika kwa ufanisi na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.
 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, alisema wizara hiyo inaendelea kusimamia na kuendeleza miundombinu na mifumo ya msingi ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10 (2024–2034).

Alisema mifumo hiyo inajumuisha mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi na makazi.

"Katika muktadha huu, utekelezaji Mfumo wa Anwani za Makazi ni hatua ya kimapinduzi inayolenga kuboresha utambuzi na utoaji huduma kwa wananchi nchini," alisema.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nadir Abdulatiff Awady, alisema uwekaji anwani za makazi kwa upande wa Zanzibar umekamilika kwa asilimia 100. Hivi sasa wanaendelea kuwahamasisha wananchi matumizi ya anwani hizo.

Awali Naibu wa Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dk. Festo Dugange, alisema kabla ya utekelezaji mfumo huo, ilikuwa ni vigumu kwa mgeni kufika katika baadhi ya maeneo ila kwa sasa imerahisishwa baada ya utekelezaji mpango huo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema Jiji la Dodoma limetenga Sh. milioni 300 kwa ajili ya kuweka kamera za CCTV katika barabara kwa ajili ya kuimarisha usalama na kuzuia wizi wa miundombinu.