Wafanyabiashara 1,520 warejeshwa Kariakoo

By Restuta James , Nipashe Jumapili
Published at 01:54 PM Feb 02 2025
Soko la Kariakoo
Picha: Mtandao
Soko la Kariakoo

MAJINA ya wafanyabiashara 1,520 watakaorejea katika Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam yametajwa na kutakiwa kwenda kujisajili kuanzia kesho hadi Ijumaa Februari 7, mwaka huu.

Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Mwinga Luhoyo, katika taarifa yake kwa umma juzi, alimtaka kila atakayeona  jina lake, kufika katika ukumbi wa Arnatoglu kwa ajili ya kujisajili kwa kujaza fomu na kufuata taratibu zinginezo za kiupangaji.

Alisema soko hilo lipo katika hatua za mwisho za kurejea kwenye biashara baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukarabati.

“lli shughuli hizo zirejee, shirika linatangaza kwa umma orodha ya wafanyabiashara 1,520 ambao wamehakikiwa na kamati iliyoundwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Mfanyabiashara anakumbushwa kufika akiwa na kitambulisho cha Taifa na namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN),” alisema.

Katika orodha ya awali, wafanyabiashara 1,170 walirejeshwa na orodha ya pili waliorejeshwa ni 350.

Maeneo ambayo wafanyabiashara hao wamerejeshwa na idadi yao kwenye mabano ni wasaidizi soko dogo (29), wasaidizi soko dogo mzunguko (49), walionunua maeneo kutoka kwa waliokuwa wapangaji (33), waliokuwa eneo la promosheni (45), wafanyabiashara waliofariki dunia na maeneo yao kurithiwa (36) na  majina ya wasaidizi (45).

Wengine ni wenye mitaji yao soko dogo ndani (45), majina ya wafanyabiashara waliopangishwa maeneo ya biashara (70), wauza mbogamboga shimoni (38) na wauza ndizi jumla soko la shimoni (15).

Pia wamo  waliokuwa kwenye vigoli sokoni Kariakoo (98), soko la wazi (194), soko dogo mzunguko (242), shimoni (322), soko la ndani (152) na soko kuu (163).

Juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo, Hawa Ghasia, alisema wafanyabiashara 366 wanadaiwa zaidi ya Sh. milioni 358 na kwamba, hawatarejeshwa hadi watakapolipa madeni yao.

Soko la Kariakoo limekarabatiwa na kuongezwa maeneo mapya baada ya kuungua Julai 10, 2021 na kuteketeza mali za wafanyabiashara. Aidha, serikali imelikarabati kwa Sh. bilioni 28.03.

Katikati ya wiki,  Rais Samia Suluhu Hassan, alipokutana na kula chakula cha mchana na watu walioshiriki uokoaji kwenye jengo la ghorofa lililoporomoka Kariakoo, Novemba 16, 2024, alisema chanzo cha kuungua kwa soko hilo ni ili kupoteza ushahidi wa kilichokuwa kinaendelea sokoni hapo.

 “Nilikuja Kariakoo na baaada tu ya kuondoka, kesho yake mkalitia moto. Baada ya kuzisema changamoto za uongozi uliokuwapo na mambo yaliyokuwa yakifanyika katika soko na kuvitaka vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi ndani ya soko, ili kupoteza ushahidi mkalichoma moto, lakini kwa ujasiri nikaamua kulijenga tena,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema juzi kwamba soko hilo litaanza kufanyakazi kwa saa 24 kuanzia Februari 22, mwaka huu.