NEMC yatahadharisha watu maeneo ya bahari na fukwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:19 PM Feb 02 2025
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi.

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka wananchi kuchukua tahadhari za kuepuka maeneo ya fukwe za bahari pamoja na miamba ya maziwa na mito ili kujinusuru na mafuriko na athari zake wakati wa mvua kubwa zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Pia NEMC imezitaka Mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa hususan Jiji la Dar es salaam kuchukua hatua stahiki kupambana na watu wanaotupa taka ngumu katika mifumo ya maji pamoja na kuhakikisha mifumo hiyo ya maji kuwa safi na kuimarisha njia na mikondo ya maji iwe safi wakati wote.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tahadhari ya mvua kubwa zinazotarajiwa kuanza kunyesha.

 

1

Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha kuwa anaweka mazingira safi na salama ili kuepusha mafuriko na mlipuko wa magonjwa ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada zetu katika ujenzi wa Taifa.


Amesema taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), zilizotolewa Januari 23 zimetabiri uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara na Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.


Aidha, amesema taarifa hiyo ya TMA iliyataja maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
2


“ (NEMC) inawatahadharisha wananchi kujiepusha kwa namna yoyote ile na vitendo vyenye kuchangia uharibifu wa mazingira kwa kuzingatia masuala kadhaa ikiwa pamoja na kuendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ili kuwa na tahadhari ya maeneo yenye viashiria hatarishi,” amesema


Amewataka wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya kandokando ya milima au miinuko mikali kuchukua tahadhari ili kuepukana na athari za maporomoko ya ardhi.


“Tunaziomba Mamlaka za Serikali za Mitaa kufuatilia kwa karibu maeneo ya uchimbaji madini na vifusi ili kuhakikisha jamii husika inakuwa salama na majanga yanayoweza kujitokeza kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha udhibiti wa taka ngumu ili zisizagae na kuingia kwenye mifereji ya maji ya mvua na mifumo ya majitaka na kusababisha kuziba,” amesema.
3


Dk Semesi amewataka abiria na wasimamizi wa vyombo vya usafiri kuwa na tahadhari wakati wa safari kwa kuzingatia kuwa maeneo ya barabara yanaweza kuwa yameathiriwa na mvua.


Amesema wananchi kwenye maeneo mbalimbali wanatakiwa kutoa taarifa kwa viongozi kwenye maeneo yao kuhusu athari zinazoweza kuwa zimejitokeza kutokana na hali hiyo.


“Wananchi wanakumbushwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, kifungu namba 57 na kuepuka ujenzi kwenye maeneo hatarishi ikiwa ni pamoja na maeneo ya kando ya mito, mabonde, fukwe za bahari na maeneo ya ardhi oevu,” amesema na kuongeza.


“Kwa kuzingatia historia ya athari za mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo mbalimbali, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuwa makini na kuchukua tahadhari zinazohitajika ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo,” amesema.
4