OFISI ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imewaita waombaji waliofaulu usaili wa nafasi za kazi mbalimbali kuchukua barua zao za kupangiwa vituo vyao ndani ya siku saba baada ya tangazo hilo.
Na Paul Mabeja, DODOMA
Taarifa ya Tangazo hilo ilitolea juzi na Ofisi ya Rais Sekretaieti ya Ajira katika utumishi wa Umma.
“Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anapenda kuwataarifu waombaji kazi wa nafasi mbalimbali waliofanya usaili kati ya tarehe 24-02-2024 na tarehe 17-01-2025 kuwa matokeo ya waombaji kazi waliofaulu usaili huo ni kama yalivyoorodheshwa katika tangazo hili,”ilisema sehemu ya tangazo hilo
Aidha, orodha ya majina hayo pia inajumuisha baadhi ya wasailiwa waliokuwa kwenye kanzidata (Database) kwa kada mbalimbali ambao wamepangiwa vituo vya kazi baada ya nafasi kupatikana.
Kadhalika, waombaji waliofaulu usaili wanatakiwa kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma zilizopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Kwenye Majengo ya Dk. Asha Rose Migiro, Masjala ya wazi ndani ya siku saba kutoka tarehe ya tangazo hili na baada ya hapo barua ambazo hazitachukuliwa na wahusika zitatumwa kupitia anuani zao za Posta,”ilisema taarifa hiyo
Vile vile, waombaji kazi waliofaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi wanatakiwa kuripoti kwa Mwajiri katika muda ambao umeainishwa kwenye barua za kupangiwa kituo cha kazi wakiwa na vyeti halisi (Originals Certificates) za masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya Ajira.
Mbali na hilo kwa wale ambao majina yao hayapo katika tangazo hili watambue kuwa hawakupata nafasi/hawakufaulu usaili, hivyo wasisite kuomba kwa mara nyingine nafasi za kazi zitakapotangazwa.
“Jambo la muhimu kwa wale wanaokuja kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi wanapaswa kuwa na kitambulisho kwa ajili ya utambuzi,”ilieleza taarifa hiyo
Ambapo vitambulisho vinavyokubalika ni pamoja na Kitambulisho cha Uraia, Hati ya kusafiria, Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, Kitambulisho cha Mpiga kura au Leseni ya Udereva.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED