Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewasihi viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia utekelezaji wa majukumu ya watendaji wa vituo wakati wa uandikishaji wa wapiga kura.
Angalizo hilo limetolewa mjini Kibaha na Kaimu Mkurugenzi wa tume hiyo, Mtibora Seleman, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa tume hiyo na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Seleman amesema kuwa tume inatarajia kuona viongozi wa vyama vya siasa wakiwahamasisha wanachama, wafuasi na mashabiki kujitokeza katika siku saba zilizopangwa kuhakiki taarifa zao, badala ya kulalamikia hitaji la kuongeza muda wa zoezi hilo.
"Haitatokea siku zikaongezwa zaidi ya hizi zilizopangwa. Hivyo, tunapaswa kutumia majukwaa yetu na mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa muda uliopangwa. Pia, tunaomba viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia majukumu ya watendaji wa vituo," amesema.
Kaimu Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa idadi ya wapiga kura 594,494 inatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwemo.
Ameeleza kuwa baada ya uboreshaji wa daftari, kutakuwa na wapiga kura 34,746,638, kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ambapo wapiga kura wapya 5,586,433 wanatarajiwa kuandikishwa. Hii ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,433 waliokuwemo kwenye daftari baada ya uboreshaji wa mwaka 2019/2020.
Tume hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa uchaguzi wa Mkoa wa Pwani kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Mpiga Kura, ambao unatarajiwa kuanza Februari 13 hadi 19, 2025.
Awali, akifungua mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk, amesema kuwa lengo la mkutano ni kuanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Pwani.
Mbarouk amesema kuwa kwa sasa tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 11 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa daftari, ambapo mzunguko huu unahusisha mikoa ya Pwani na Tanga.
Ameeleza kuwa awali, zoezi hili lilianza katika mikoa mitatu—Kigoma, Tabora, na Katavi. Hadi sasa, tume imeshakamilisha uboreshaji huo katika mikoa 25, ikiwemo mikoa mitano kutoka Zanzibar.
Kwa Mkoa wa Pwani, tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 186,211, ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 992,067 waliopo kwenye daftari la kudumu. Hivyo, baada ya uandikishaji, idadi ya wapiga kura mkoani humo itafikia 1,178,278.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED