Kamati yaundwa kuchunguza wageni wanaofanya umachinga Kariakoo

By Joseph Mwendapole , Nipashe Jumapili
Published at 06:00 PM Feb 02 2025
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo
Picha: Mtandao
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, ameunda kamati maalumu ya watu 15 kuchunguza wingi la wageni kufanyabiashara za uchuuzi ‘Umachinga’ katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Hatua hiyo inatokuja baada ya mwishoni mwa wiki, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kusikia kilio cha Watanzania hususan wafanyabiashara wa Kariakoo, kuhusu kero hiyo.

Dk. Jafo alisema kamati hiyo itakayokuwa chini ya Mwenyekiti wake,  Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda  Lwoga, itafanya kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja na kuwasilisha taarifa yake.

Alitangaza hayo, jijini Dar es Salaam, jana, alipokutana na wafanyabiashara wa Kariakoo akiwemo  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Hamis Livembe, Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo na  Halmashauri Kuu ya uongozi wa soko hilo.

“Hivi karibuni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokea kilio cha wananchi wa Kariakoo, Dar es Salaam na Watanzania hususan wafanyabiashara, suala la hivi sasa kuwepo kwa mwingiliano wa wageni wengi ambao huwa wanakuja na ajenda ya uwekezaji, kwa bahati mbaya uwekezaji wao hauakisi suala zima la uwekezaji,” alisema.

“Wanapofika nchini changamoto iliyojitokeza ni kwamba, wanashiriki katika shughuli nyingine ambazo zipo nje ya utaratibu wa uwekezaji,” alisema.

“Baadhi ya shughuli hizo hususan ni kufanya biashara za rejareja za kimachinga, mwisho wa siku huathiri mwenendo wa biashara kwa Watanzania,” alisema.

Waziri huyo alisema hiyo  imekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara na kuathiri biashara zao huku ikizingatiwa Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni ambapo mgeni yoyote au mtu anapaswa kufanyabiashara kulingana na maelekezo ya serikali.

“Kuna wingi la wageni ambao wanafanya biashara tofauti na utaratibu wa kisheria, hivyo huleta kero kwa wafanyabiashara wazawa na kuathiri mitaji yao na kuwa na vijana waliofilisika kutokana na wengine wameanzisha magodauni na kuleta biashara na kuuza rejareja,” alisema.

Alisisitiza kuwa, jambo hilo halivumiliki, hivyo anatekeleza maelekezo ya Rais Dk. Samia akiwa waziri mwenye dhamana kwa kuunda kamati maalumu ya  watu 15, kuondoa changamoto hiyo inayowakabili wafanyabiashara.

Dk. Jafo alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Edda anaamini atasaidia kwa kuwa amebobea upande wa biashara, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa wizara hiyo, Sempeho Manongi (Katibu wa Kamati).

Wajumbe ni Naibu Kamishna wa Polisi, Francis Maro, Naibu Kamishna Uhamiaji, Kigongo Shile, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade),  Latifa Khamis.

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya ushindani nchini (FCC), William Erio, Teddy Frank, Zubeda Masoud, Ofisa Kazi Mwandamizi wa Dar es Salaam, Eliuluma Mabelia, Raphael Maganga kutoka sekta binafsi, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Hamis Livembe.

Alitaja miongoni mwa hadidu za rejea ni utafiti wa kina Soko la Kariakoo likiwa kama la mfano, kubaini ukubwa wa tatizo la wageni kufanya biashara nchini ambalo linaathiri ajira kwa Watanzania. 

Pia  watakagua vibali vya wageni na uhalali wake, kuchunguza wageni kupewa vibali na leseni za biashara zinazofanywa na Watanzania.

Dk. Jafo alisema kamati hiyo itaangalia masuala ya dharura ni nini kifanyike kwa haraka kutatua tatizo hilo kwa kuainisha njia za haraka na muda mfupi, chanzo cha tatizo na namna ya kuepuka.

Aliwaomba wafanyabiashara kuwa watulivu wakati kamati hiyo inafanya kazi yake ambayo itasaidia siyo tu sekta ya biashara bali na nyingine kuweka misingi ya utekelezaji.