RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na kuahidi kuwa serikali itapitia upya maslahi ya kada ya walimu ili kuipa hadhi inayostahili.
Pia amesema serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na mwelekeo wa sera hiyo.
Akizungumza jana jijini hapa, Rais Samia alisema pamoja na uhitaji wa rasilimali na miundombinu ya elimu, kiungo kikubwa katika utekelezaji huo ni mwalimu.
Kwa maoni yangu (mwalimu) ndiye kiongozi wa elimu, hivyo katika maboresho haya, lazima mwalimu awe katikati ya mduara wa maboresho yetu. Tutapitia upya maslahi ya kada ya walimu nchini ili kuipa hadhi inayostahili kama mama wa taaluma zote duniani.
“Niitake TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kuandaa mkakati wa kutekeleza sera hii kwa upande wa miundombinu,” alisema. Rais Samia aliziagiza Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwezesha na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitaala mipya ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Kuhusu sera hiyo, alisema elimu itakuwa ya lazima kutoka miaka saba na kuwa 10 na kwamba hiyo ilitokana na wanafunzi kumaliza elimu ya msingi wakiwa na umri wa miaka 13, hivyo kukosa sifa ya kuajiriwa na kujiajiri.
Pia alisema wanakuwa hawana elimu ya ufundi hivyo kwa sasa kupitia sera hiyo, itamwezesha kijana kuingia kwenye uzalishaji. Alisema sera hiyo inajibu hoja ya muda mrefu ya kuweka mfumo wa kutoa na kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo ulioko.
Aidha, alisema somo la ujasiriamali litakuwa la lazima kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, ili kumpa misingi ya biashara na kujifunza Lugha za Kiingereza, Kichina, Kifaransa na Kiarabu, kwa kuwa ndizo zinazoendesha uchumi duniani.
Awali, Rais Samia alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 yakiwamo serikali imejenga shule za msingi 1,649 na shule mpya za sekondari 1,042 na zimeongeza fursa za elimu kwa watoto, huku vyuo vya ufundi stadi (VETA) vikijengwa kwenye mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe na Rukwa.
Ujenzi wa vyuo vya VETA, alisema unaendelea kwenye mkoa wa Songwe na wilaya 64 na kwamba uwekezaji huo unawapunguzia mzigo wananchi waliokuwa wanalazimika kusafiri kwenda wilaya zingine kutafuta ujuzi.
Alisema bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 467 hadi 787 na wanufaika wameongezeka kutoka 149,508 hadi 220,376 mwaka 2023/24. Hata hivyo, Rais Samia alisema idadi ya wasiojua kusoma na kuandika imepungua kutoka asilimia 70 mwaka 1960, hadi sasa wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 83.
Kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), alisema ni lazima kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi wa masuala hayo na kuangalia matumizi hayo yasiwapeperushe na utovu wa maadili.
“Mbele yetu ninaona mahitaji makubwa ya ajira kwa vijana yataendelea kuongezeka mbele ya safari kwa sababu kubwa tatu, ambazo ni kasi ya mabadiliko ya teknolojia itakayosababisha baadhi ya kada kukua na zingine kutoweka na zile zitakazosalia hazitahitaji watu wengi,” alisema.
Alitaja sababu nyingine ni utandawazi na ongezeko la idadi ya watu isiyoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi kwa ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka ifikapo 2044, idadi ya watu nchini itakuwa milioni 123.
“Ninachokiona mbele kinahitaji tuwe na maandalizi ya kutosha kwa kuzingatia ubora wa elimu yetu kwa kutoa elimu bora zaidi na kuandaa vizuri zaidi vijana wetu kumudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa au kujiajiri,” alisema.Rais Samia alisema utekelezaji wa sera umeanza kuonesha mwelekeo mzuri kwa kuwajengea umahiri na ujuzi vijana kwenye ufundi.
“Wataalamu wetu wamechambua vizuri mwenendo wa uchumi wetu, mwelekeo wa dunia, kasi ya maendeleo ya dunia na kujifunza kutoka kwa wenzetu. Dhamira yetu ni kumwandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki kukabiliana na ushindani na anufaike kiuchumi,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alisema sera hiyo itawezesha kubadilisha mfumo wa elimu ili kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa teknolojia.
Alisema utafiti unaonesha sera ya elimu haiakisi mabadiliko ya teknolojia, kunakuwa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa sababu nguvu kazi isiyokuwa na ujuzi inazalishwa kwa wingi kuzidi mahitaji.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema asilimia kubwa ya mambo yaliyokuwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambayo ilizinduliwa mwaka 2015, hayakutekelezwa na kumpongeza Rais Samia kwa kufanikisha uboreshaji wa sera na mitaala mipya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alisema bodi ya shirika hilo kuanzia mwaka 2013 hadi sasa, imechangia miradi ya maendeleo ya elimu yenye thamani ya Sh. bilioni 518.
Alisema ukaguzi uliofanyika na shirika hilo kwenye miradi hiyo nchini, umeridhika kuwa fedha hizo zinatumika vizuri na ndio maana wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika awamu nyingine ya tatu.
Kikwete alisema tayari mazungumzo ya awali katika awamu ya tatu yameanza kati ya serikali na GPE ambapo Dola milioni 88.56 zimeshatengwa na nyingine Dola milioni 50 ziko tayari kujumuishwa kwenye mpango huo.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuwapo na ubora wa elimu inayotolewa Bunge lipo tayari kufanya marekebisho ya sheria zitakazoonekana haziendani na sera hiyo mpya.
Alishauri baada ya kuzinduliwa kwa sera ni muhimu kuangalia masomo ambayo hayahitajiki tena kwa kuwa watoto wanauwezo wa kufahamu bila kufundishwa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Leila Mohamed Musa, alisema kwa upande wa Zanzibar, mapitio ya mtaala wa mafunzo ya amali yameanza ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sera na kwamba, matayarisho ya mafunzo kwa ajili ya walimu yamekamilika na kuanza kutolewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED