CHAMA cha Tanzania Labour Party (TLP), kimemchagua Richard Lyimo, kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho atakayeongoza kwa miaka mitano ijayo huku wanachama 21 wakifukuzwa uanachama.
Ikumbukwe kuwa tangu alipofariki aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Agustino Mrema, mwaka 2022, nafasi hiyo ilikuwa inakaimiwa na Hamad Mkadamu.
Lyimo alichaguliwa katika mkutano mkuu wa Chama cha hicho, uliofanyika jana Dar es Salaam ukijumuisha wajumbe 84.
Katika uchaguzi huo, Lyimo alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo ya Mwenyekiti na kabla ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo mpya, alikuwa Katibu Mkuu wa TLP.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, aliyechaguliwa ni Johari Hamis, ambaye naye katika kinyang`anyiro hicho alikuwa mgombea pekee.
Kadhalika, mkutano huo kwa kauli moja, uliridhia kuwafuta uwanachama, wanachama 21 wa chama hicho, wakiwamo viongozi wanaodaiwa waliofanya majaribio ya kuandaa mikutano miwili ya kuchaguana kinyume cha chama chao hicho kwa ajili ya kuziba nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Mwenyekiti wa chama hicho Agustino Mrema, aliyefariki mwaka 2022.
Miongoni mwa wanachama na viongozi waliofukuzwa uanachama ni Dominata Rwechangura ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho, Ivan Maganza, aliyekuwa Mwenyekiti wa vijana taifa wa chama hicho na Mariam Kassin.
Wengine waliofukuzwa ni Riziki Nganga, Stanley Ndumagoba, Mary Mwaipopo, Mohamed Mwinyi, Laurian Kazimiri, Nataria Shirima, Kinanzaro Mwanga, Godfrey Stivin na Rashid Amiri.
Pia, wapo Twaha Hassan, Tunu Kizigo, Damari Richard, Hamad Alawi, Mohamed Hemed, Mariam Hamis, Mussa Fundi, Mwajuma Mussa na Osward Nyoni.
Baadhi ya wanachama waliofukuzwa walipoulizwa, walikana kuutambua mkutano huo wakidai haukufanyika kisheria huku wakisisitiza kuwa wao bado ni viongozi.
Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza, alithibitisha kwamba mkutano huo uliomchagua Lyimo na wenzake pamoja na kuwafukuza baadhi ya wanachama hao ulifanyika kihalali.
Pia, aliwata wenye malalamiko kuhusiana na chochote kilichofanyika katika mkutano huo, wampelekee malalamiko yao.
“Mkutano ulifanyika kihalali na aliyeuitisha anatambuliwa kikatiba na taratibu za chama chao na walishatoa taarifa, kwa hiyo yote yaliyofanyika ni halali na yana baraka kutoka kwa wajumbe wa mkutano, wenye malalamiko waniletee kwa kufuata utaratibu, nitayashughulikia,”alisema Nyahoza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED