Serikali yafunguka upatikanaji ARV, yasisitiza kuwa haziuzwi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:49 AM Feb 09 2025
D
Picha: Mtandao
D

WIZARA ya Afya imetoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji dawa za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV), ikieleza kuwa zipo za kutosha na haziuzwi.

Jana, Nipashe iliripoti kuhusu madai ya baadhi watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) wanaotumia dawa hizo, wakieleza kwamba wametaarifiwa wataanza kuzinunua hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Roida Andusamile, ilifafanua kuwa mikakati ya serikali ni kuendelea kuwahudumia WAVIU kama kawaida.

"Serikali kupitia wizara inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki, ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

"Watumiaji dawa hizi, hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji dawa hizo," alisema.

Alisema hakuna uhaba wa ARV na kwamba wananchi hawapaswi kuwa na hofu kwa kuwa serikali itaendelea kuwahudumia kama kawaida.

"Serikali kupitia Wizara ya Afya, inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa dawa za kufubaza (kupunguza) makali ya Virusi vya UKIMWI haziuzwi na kwamba zipo za kutosha," alisisitiza.

Alifafanua kwamba wananchi wanapaswa kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya, ili kuzuia usugu wa vimelea vya ugonjwa huo dhidi ya dawa.

Juzi, Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA), kupitia Eva Philipo, liliiambia Nipashe kwamba kwa sasa ARV zinatolewa bila malipo, lakini wametaarifiwa kuwa zitaanza kuuzwa, japokuwa hawajaelezwa ni lini utekelezaji wake utaanza.