Yanga kicheko sare ya Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 12:26 PM Feb 09 2025
Ofisa Habari wa Klabuya Yanga, Ali Kamwe
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Klabuya Yanga, Ali Kamwe

KLABU ya Yanga imeweka wazi kuwa imefurahia mno sare ambayo watani wao wa jadi Simba waliipata Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, mkoani Manyara dhidi ya Fountaina Gate, ikisema imewaongezea nguvu na morali ya kupambana kwa ajili ya kuutetea ubingwa wao.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema jana kuwa, sare hiyo imewafanya sasa kuongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu vizuri zaidi tofauti na awali ambapo walikuwa wakiongoza kwa muda na kushuka nafasi ya pili kila watani zao walipokuwa wakishinda.

"Tumefurahishwa na sare ya Simba, imetuweka kwenye nafasi ya kwanza vizuri. Matokeo yale ya sare kati ya Fountain Gate na Simba yamekuwa na faida ya kukaa nafasi ya kwanza bila utata. Sawa japokuwa tunafurahi, lakini furaha hii ituongezee hamasa kubwa na umakini, sasa kampeni yetu ni kuhakikisha tunabaki kileleni mpaka mwisho, kila mechi sasa inabidi tucheze kama fainali," alisema Kamwe.

Katika mchezo huo, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 huku Ladack Chasambi akijifunga mwenyewe alipokuwa akimrudishia mpira golikipa wake, Moussa Camara.

Ni matokeo yaliyoifanya Simba kushindwa kukwea tena kileleni na kubakia na pointi 44 kwa michezo 17 iliyocheza, ikiiacha Yanga kileleni ikiwa na pointi 45.

Hata hivyo, pamoja na furaha, Kamwe alitoa angalizo kuwa michezo ya Ligi Kuu bado ni mingi na chochote kinaweza kutokea mbele, hivyo kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuungana na kuipa sapoti timu yao.

"Ligi bado mbichi sana, huwezi kusema tumeshakuwa mabingwa, kuna mechi nyingi mbele za kucheza ambapo chochote kinaweza kutokea, ili kuepuka hayo kama taasisi inabidi tuwe imara kuanzia viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki, wote tuungane ili kuutetea ubingwa wetu wa ligi," alisema.

Kamwe, alisema wanakwenda katika mchezo wa Jumatatu kucheza na JKT Tanzania kwa nguvu zote na tahadhari ya hali ya juu.

"Tutakwenda kucheza kwa nguvu zote na tahadhari ya hali ya juu dhidi ya JKT Tanzania, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, tunajua mechi itakuwa ngumu kwa sababu tunakwenda kucheza na timu ambayo msimu uliopita tulitoka nayo suluhu kwenye uwanja wao," alisema Kamwe.