Simulizi; Rais Nujoma kuitwa Sam Mwakangale

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 08:47 PM Feb 09 2025
Sam Nujoma
Picha: Mtandao
Sam Nujoma

WAKATI nchi ya Namibia ikiomboleza kifo cha Rais wa Kwanza wa taifa hilo tangu kupata uhuru wake, Sam Nujoma, mwonekano wake na kimo chake kama John Mwakangale, miongoni mwa sababu za kiongozi huyo kuitwa ‘Sam Mwakangale’.

Nujoma (95), amefariki dunia jana, jijini Windhoek nchini humo, akiwa ni miongoni mwa wapigania uhuru na wanaharakati wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, walioungwa mkono na Mwalimu Julius Nyerere.

Sam Nujoma
Alipofika nchini, miaka 1969 mkoani Dodoma na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Dodoma, John Mwakangale, walikubaliana kutumia jina lake kuwa Sam Mwakangale, ili kujilinda asiuawe. Nujoma alikuwa miongoni mwa wapigania uhuru waliofika nchini kupanga harakati za ukombozi za nchi zao, wakiwamo Nelson Mandela na Kanyama Chiume wa Malawi.

John Mwakngale akishiriki harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na Mwalimu Nyerere na TANU ilipoasisiwa alichaguliwa na kuonyesha mchango mkubwa kisiasa na harakati hizo ilimfanya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) mwaka 1957.

Mwalimu Julius Nyerere (kuli) na John Mwakangale, mwaka 1972, Mbeya. (Picha: JBM)
Akizungumza na Nipashe leo, mtoto wa kwanza wa mwanasiasa mkongwe John Mwakangale, Stephen Mwakangale, anasema anakumbuka baba yake akiwa Mkuu wa Mkoa Dodoma, Nujoma alipokewa katika kambi ya wakimbizi na kuungana na wapigania uhuru kutoka maeneo tofauti.

“Wapigania uhuru wote walikuwa wanapewa majina, majina waliyotumia hayakuwa ya kwao. Sababu ni kuwalinda dhidi ya wakoloni na maadui wengine, ili mipango yao ya kupigania nchi zao itimie. Baba alimpokea kama mdogo wake au mwanawe. Wapigania uhuru walifikia kambi ya Kongwa, Mzee alienda kutembelea mara kadhaa akiwa mkuuu wa Mkoa Dodoma.

Hati ya kusafiria ya Sam Nujoma ikiwa na jina Sam Mwakangale
“Nakumbuka baba (John Mwakangale) akiwa Mkuu wa Mkoa Dodoma, alimpokea katika kambi ya Kongwa. Lakini vilevile baba alifanana mwonekano kwa kiwango fulani na Nujoma, kwa kimo na maumbile. Ndipo akaamua kumruhusu atumie jina lake yaani ‘Sam Mwakangale,” alisema Stephen.

Alisema kambi hiyo na nyinginezo kama vile Mazimbu mkoani Morogoro, zilitengwa maalum kwa ajili ya kuwapokea wageni wa aina hiyo, ambao walitoroka nchi zao na kuja kupanga mipango ya kupata uhuru.

“Kwa kiwango kikubwa mbinu za kivita katika kufanikisha malengo yao, walijifunza hapa, hata Nelson Mandela akitokea Afrika Kusini, alipita hapa, alipokelewa na baba (John Mwakangale) Mbeya, akamfanyia mpango wa kumsafirisha kuja kuonana na Nyerere, Dar es Salaam, kwenda Addis Ababa,” alisema Stephen.

“Nakumbuka hata Kikwete (Jakaya), alikuwa akimtumia mara kwa mara kadi za salamu za sikukuu mzee na pia Kikwete aliwahi kumwelezea Nujoma alipofika hapa nchini kuaga, akasema aliitwa Sam Mwakangale, kwa sababu maalum,” alisema.

“Kutumia jina la Sam Mwakangale, alionekana kuwa ni Mtanzania, ikawa rahisi kusafiri kwenda nje ya nchi bila kusumbuliwa. Hati ya kusafiria ya kwanza ya Nujoma, aliipata Tanzania na  jina lake linasoma ‘Sam Mwakangale’ lengo likuwa kumlinda, asiuawe.

Sam Nujoma na Nelson Mandela
“Hata Kanyama Chiume wa Malawi, alifika na kulala nyumbani kwetu Makandana (Tukuyu, Mbeya), kwa harakati kama hizo. Lakini wote hao walielekezwa na Mwalimu Nyerere ili kufika kwa mzee,” alieleza Stephen.

SAMIA AOMBOLEZA

Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Wanamibia kutokana na kifo cha Baba wa Taifa hilo na Rais wa Kwanza wa Namibia, Sam Nujoma.

“Nimesikitishwa sana kupata habari za msiba wa Rais wa Kwanza na Baba Mwanzilishi wa Taifa la Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dk. Sam Nujoma.

“Mpigania uhuru, Mwana-Pan-Africanist, na rafiki wa dhati wa Tanzania ambako aliwahi kuishi wakati wa harakati za uhuru wa Namibia.

Dk. Nujoma aliishi maisha ya kujitoa kwa huduma, ambayo hayakubadilisha hatima ya nchi yake pekee, bali pia yaliwahamasisha vizazi kusimama kidete kwa ajili ya maadili ya uhuru, usawa na haki.

Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natuma salamu za rambirambi za dhati kwa Mheshimiwa Dk. Nangolo Mbumba, Rais wa Jamhuri ya Namibia, wananchi wa Namibia, Mama Mwanzilishi wa Kwanza wa Jamhuri ya Namibia, Kovambo Nujoma; watoto wa Dk. Nujoma, familia yake yote, marafiki na wapambanaji wenzake wa SWAPO, Roho yake na ipumzike kwa amani.” alisema Rais Samia.

KIFO CHA NUJOMA

Kifo cha Sam Nujoma kimetangazwa jana na Rais wa Namibia, Dk. Nangolo Mbumba, huku akisema nchi itatangaza maombolezo ya kitaifa.

Rais huyo alisema kifo cha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Namibia na Baba Mwanzilishi wa Taifa, Mheshimiwa Dk. Sam Shafiishuna Nujoma, kimetokea jana, alikokuwa amelazwa hospitalini kwa matibabu na uangalizi wa kitabibu kutokana na maradhi.

“Kwa bahati mbaya, safari hii, shujaa wetu mkubwa wa taifa hili hakuweza kupona. Kwa hivyo, kwa huzuni kubwa na masikitiko, natangaza asubuhi hii ya Februari 9, 2025 kwa watu wa Namibia, ndugu na dada zetu wa Afrika na ulimwengu kwa ujumla, kuhusu kifo cha mpigania uhuru wetu na kiongozi wetu wa mapinduzi

Dk. Sam Shafiishuna Nujoma. Rais Nujoma ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 95 mnamo tarehe 8 Februari saa 23:45 huko Windhoek, Namibia. Baba yetu Mwanzilishi aliishi maisha marefu na yenye mchango mkubwa.

“Alilitumikia taifa lake kwa upekee. Aliongoza kwa ushujaa watu wa Namibia katika nyakati ngumu zaidi za mapambano ya ukombozi, hadi kufanikisha uhuru na kujitawala Machi 21, 1990.

Kama Rais wa Kwanza, Dk. Sam Nujoma alitoa uongozi wa hali ya juu kwa taifa letu na hakusita kuwahamasisha Wanamibia wote kujenga nchi itakayojivunia hadhi yake miongoni mwa mataifa mengine duniani.

Katika mwamko huo, kiongozi wetu mashuhuri, Dkt. Nujoma, hakutuongoza tu kuelekea uhuru bali pia alitufundisha kusimama imara na kuwa mabwana wa ardhi hii kubwa ya mababu zetu.

Katika kipindi hiki cha maombolezo ya kitaifa, tunapaswa kupata faraja kutokana na uongozi wake usio na kifani na mchango wake wa kipekee kwa mapambano ya ukombozi, maendeleo, na umoja wa watu wa Namibia.

Ningependa kutoa shukrani zangu kwa wahudumu wa afya waliomhudumia kwa bidii kiongozi wetu mpendwa. Pia, natoa shukrani kwa Wanamibia na marafiki wa Namibia waliotuma salamu na maombi ya kumtakia afya njema Baba yetu Mwanzilishi na Rais wa Kwanza, Dk. Sam Shafiishuna Nujoma.

Kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Namibia, ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa Mama wa Kwanza Mwanzilishi wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Kovambo Nujoma, Utoni Nujoma, watoto wao, pamoja na familia nzima ya Nujoma na Kondombolo.

Baada ya mashauriano na familia ya Nujoma na Kondombolo, Serikali ya Jamhuri ya Namibia itatangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa na mipango ya mazishi,” ilisema taarifa ya Rais Mbumba.