RC Macha ahamasisha wananchi kupima TB

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 01:24 PM Feb 09 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza wakati wa kuzindua kampeni ya upimaji wa ugonjwa wa Kifua kikuu.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza wakati wa kuzindua kampeni ya upimaji wa ugonjwa wa Kifua kikuu.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo, kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa wa Kifuakikuu (TB), kwa kuwa matibabu yake yatatolewa bure.

Amebainisha hayo jana, wakati akizindua Kampeni Harakishi ya Kuibua Wagonjwa Wenye Vimelea vya Ugonjwa wa Kifua kikuu.

Amesema kupitia kampeni hiyo, wananchi wajitokeze na watakaobainika kuwa na ugonjwa huo, waanze kupata matibabu ambayo hutolewa bure kuanzia vipimo hadi dawa.

“Mkoa huu wa Shinyanga watu wenye tatizo la ugonjwa wa Kifua kikuu wapo 2,903 huku watu 1,349 bado hawajafikiwa, ambao ndiyo wanatafutwa kupitia kampeni hii.  Ugonjwa huu ni hatari una ambukizwa kwa njia ya hewa,” amesema Macha.

Amesema kwamba mtu mmoja mwenye tatizo hilo, kwa mwaka mmoja anaweza kuambukiza watu 20 na kwamba hatua zisipochukuliwa mapema tatizo litakuwa kubwa, ndiyo maana serikali inaendesha kampeni hiyo, ili kuokoa afya za wananchi. 

Aidha, amewataka wananchi wanapotumia dawa za Kifua kikuu wamalize dozi na siyo kukatisha hali ambayo inasababisha ugonjwa kuwa usugu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, amesema kwa takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2023, watu milioni 10.8 waligundulika kuwa na ugonjwa huo na milioni 2.5 walifariki dunia.

RC Macha ahamasisha wananchi kupima TB
Amesema ugonjwa huo kwa asilimia 45 unaathiri nchi za Asia huku 24 kutoka Afrika na kwamba tafiti zinaonyesha kati ya watu 100, watu 25 wana tatizo la Kifua kikuu.

Ametaja dalili za ugonjwa huo, kuwa ni kukohoa muda wote, homa za muda mrefu, mwili kupungua uzito, kutokwa jasho hasa nyakati za usiku na huambukizwa kwa njia ya mfumo wa hewa.

Dk.Luzila ametaja aina za TB, kuwa ipo ya moyo, mifupa ya mgongo, ubongo na mapafu,

“Takwimu za mwezi Januari ambazo tulipima watu 84, watu sita waligundulika kuwa na vimelea vya Kifua kikuu. Februari tulipima pia watu 28 na watu watatu, walikuwa na vimelea Kifua kikuu na walianza kupata matibabu,” amesema Dk. Luzila.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile, amesema kampeni hiyo lengo ni kufikia watu 1,349 ili wapate tiba na wasiambukize.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Salamu Hamduni, amesema kampeni hiyo ni endelevu, na huduma zake ni bure na inaratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wa kupambana na ugonjwa huo.

Baadhi ya wananchi wa mkoani hapa,  akiwamo Magera Seni, ambaye amejitokeza kupima vimelea vya ugonjwa, ameishukuru serikali kwa kampeni hiyo, ambayo imelenga kuokoa afya za wananchi.