Ushuhuda wa kutisha mchawi akimwaga siri

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 05:26 PM Apr 07 2024
Mchawi amwaga siri.
PICHA: MAKTABA
Mchawi amwaga siri.

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee kupata mauzauza ya dunia yetu hii. Wachawi waanza kutoa siri zao hadharani baada ya mambo kuwawia magumu. Sikiliza ushuhuda huu ufungue macho yako ya kimwili na kiroho.

Watu wengi wamekuwa wakipuuzia kuhusu habari za uchawi eti kwamba haupo. Wanaugua, wanaachishwa kazi, wanakosa kazi, wanafilisika japo walikuwa matajiri wakubwa. Mbaya zaidi, wanakufa vifo vya ghafla. Lakini bado wanaona ni matukio ya kawaida kumbe chanzo ni maadui waliojificha.

Adui aliyejificha ni hatari kuliko mtu anavyofikiri. Yule adui unayemjua na kumwona ni rahisi kumshughulikia, hata kumkwepa kwa tahadhari. Mara nyingi nimeeleza hapa kwamba kuna ulimwengu wa aina mbili, huu unaoonekana kwa macho ya mwili na ule wa roho usioonekana.

Ulimwengu usioonekana ndio hatari zaidi na ndiko chimbuko la matatizo yote. Huanzia huko ndiko matatizo yakajidhihirisha kwa kuyaona kwa macho ya mwili.

Leo tuweke suala la ndoa kando tukisubiri maoni kwa tuliyojadili wiki zilizopita. Tuangaze  sarakasi za wachawi katika ulimwengu wa roho (ule uliojificha), hauonekani lakini yanayofanyika huko ni makubwa na ya kutisha.

Wiki moja iliyopita nilihudhuria kongamano la injili pale viwanja wa Biafra, Kinondoni mkoani Dar es Salaam. Kiongozi wake alikuwa Mchungaji Ezekiel kutoka Kenya. Ni kongamano la siku nne lililokuwa na miujiza na shuhuda mbalimbali.

Ushuhuda ulionigusa sana ni baba mmoja wa hapa Tanzania aliyejisalimisha Machi 22, mwaka huu, akaelezea mambo ya kichawi aliyofanya katika maisha yake hadi kusababisha kukatwa mguu baada ya kukiuka masharti kwa wakuu wake wa kichawi.

Hebu sikia sehemu ya maelezo yake niliyobahatika kuyanasa ili ujue wachawi wapo na wanafanya mambo makubwa ya kutisha. Bwana huyu anasema hivi;-

“Ndugu zangu waliniloga sana. Wakaniambia mtoe mtoto wako wa kwanza, ama mama yako au baba yako. Lakini mimi niliposhirikishwa jambo hilo nilikataa. Baada ya kukataa ndugu zangu waliniloga sana.

“Baada ya hapo walinishambulia sana wachawi, wakadai kwamba kila baada ya mwaka nitakuwa naletewa gunia 20 za mahindi, gunia tano za maharage na Sh. 500,000 kila mwaka. Lakini bado  nilikataa kwa sababu walitaka niwe mwenyekiti ili niweze kutoa sadaka ya watoto. Lakini kwa bahati nzuri kwa sababu katika ukoo wetu tulikuwa  wachawi wakubwa. Ndiyo maana wale walinitamani ili niwe mchawi katika kikundi chao.

“Na bahati nzuri katika kuishi, nilizaliwa nikakuta chui, simba, chatu, nyoka weusi, nyuki wa ndani. Nyuki nilikuwa nawafuga ndani, halafu na vyura waikubwa sana ambao wakilia tu najua kwamba kesho lazima mvua inyeshe. Wakilia tangu asubuhi hadi jioni, najua kesho itanyesha mvua ya mafuriko na wakilia mara moja, najua kwamba kesho kutakuwa na mvua za muda wa saa moja.

Alipoulizwa na Mchungaji Ezekiel kwamba wanyama hao walikuwa wanakula nini akasema; “Nyoka wanakula unga na mimi ndiye ninayewapa. Ezekiel: Ulikuwa na nyoka wangapi? Akajibu alikuwa na nyoka wengi sana.

Akasema vyura walikuwa wanakula wadudu na walikuwa wanaishi chini ya kitanda na chini ya mtungi wa maji. Nyoka niliwajengea nyumba ya milango minne. Simba na chui tulikuwa tunamchinjia kondoo, mbuzi mweupe na kuku mweupe kila baada ya mwaka.

Simba alikuwa anakula kwa mwaka na alikuwa anafanya mawindo kwani wakati nazaliwa chui, nyoka walikuwa  silaha kwa ajili ya vita kwa sababu mimi nilizaliwa katika familia ya kitemi.

Kukiwa na vita anaenda simba, chui au nyuki. Hivyo ni vita vya kiuchawi pale ufalme na ufalme ukitaka kugombana ulimwengu wa giza. Tunatuma simba au nyoka au nyuki. Lakini kwa bahati nzuri mimi nilianza kuwatumia kwa kwa kulipiza kisasi.

Mtu akija kunipa Sh. milioni mbili au tatu basi natumia nyuki au fisi. Lakini kwa bahati mbaya mwaka 2018 mwezi wa 11 nikawa nimeugua kiuno, nikachomwa sindano. Baada ya muda tatizo likatokea, damu ikavimba kuanzia kiunoni upande wa mguu ule uliochomwa sindano. Nikapata kitu walichoita ni ‘gangri’, nikakatwa mguu.

Msomaji wangu, fuatilia wiki ijayo mambo mazito mbele. Baada ya kukatwa mguu, nini kiliendelea? Tafuta nguvu ya Mungu mpendwa kudhibiti wachawi. Je, una maoni, kisa? Ujumbe 0715268581. Namba ipo pia WhatsApp.