MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amefafanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu uliohusu eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya maakaburi kuvamiwa na kujengwa nyumba za makazi ya watu.
Eneo lipo Kimani Mtaa wa Kinyamwezi, Kata ya Pugu, Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo wakazi wa eneo hilo walimtuhumu Elizabeth Mwakapangala kuliuza huku akifukua makaburi bila ya kufuata sheria.
Mpogolo akizungumza na wananchi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 13, 2026 ambao ulihudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuhuruma Mabelya alithibitisha eneo hilo lilitengwa na Serikaali kwa ajili ya makaburi.
“Eneo hili lenye ramani ya upimaji namba E' 351\96, ya mwaka 2000, Kiwanja Na. 423 Kitalu N Pugu Mwakanga Kata ya Pugu Halmashauriya Jiji la Dar es Salaam lilitengwa kwa matumizi ya makaburi kwa mujibu wa mipango miji, lakini baadhi ya yetu yaani Elizabeth ambaye alikuwa msimamzi wa mirathi ya Saidi Shomari alifungua kesi ya ardhi namba 202/2020 dhidi ya Halmashauri ya Jiji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mahakamani,” alisema Mpogolo.
Hata hivyo mpogolo alisema hukumu iliyotolewa na mahakama na Jaji A. M. Msafiri aliyesikiliza kesi hiyo ilielekeza mlalamikaji Elizabeth alipwe fidia na siyo kuuza eneo la makaburi wala kufukua makaburi ya watu na kutupa mabaki ya miili hiyo dampo kama alivyofanya.
Aidha, alisema Jaji huyo alitoa mwongozo mzuri kwa mlalamikaji wa namna ya kupata haki yake ya fidia na kueleza kuwa Mahakama haina mamlaka ya kufuta ramani ya mipango miji iliyoandaliwa na Serikali au kuhoji mamlaka ya Rais ya kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma.
Kufuatia hukumu hiyo, Mpogolo aliwaeleza wananchi hao, mlalamikaji hakuwa na haki ya kuuza eneo hilo wala kuhamisha makaburi na nikinyume na katazo la Sheria ya Mipango Miji katika Kifungu cha 3 (e) cha sheria hiyo.Alisema uhamishaji wa makaburi upo kwa mujibu wa sheria za nchi na kueleza kuwa mtu yeyote hawezi akatoka na maamuzi ya kikao cha familia na kwenda kuhamisha mwili wa mtu aliyezikwa kwenye kaburi husika ni lazima afuate utaratibu uliopo kisheria na miiko ya dini zetu.
Alisema mlalamikaji Elizabeth anapaswa kufuata utaratibu wa kisheria ili apate haki yake na si vinginevyo.
Mpogolo alisema awali mlalamikaji alisimamishwa kufanya chochote kwenye eneo hilo analodai ni lake lakini hakufuata maelekezo na sasa Serikali imekata rufaa uamuzi wa Mahakama na kuhusu kufukua Makaburi na kutupa mabaki ya miili wanakwenda kushughulika naye kwa mujibu sheria.
Aidha Wananchi hao wamedai kuwa eneo lenye mgogoro lilitengwa kwa ajili ya maziko, kama walivyoelekezwa na serikali ya mtaa na watu waliohamishwa kutoka Kipawa kupisha upanuzi wa Uwanjani wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake Elizabeth, alikanusha madai hayo akieleza kuwa hajawahi kufukua makaburi hayo na kwamba eneo hilo siyo eneo la Makaburi na ni mali yake halali ambalo anazo nyaraka zote baada ya kushinda kesi mahakamani Oktoba 20, 2022.
“Nilishinda kesi nikarudi nikawa nawazuia wananchi viwanja na wengine wakawa wanaendelea na ujenzi wakati wanaendelea akaja Kasimu Mfinanga aliyekuwa shahidi upande wakati wa kesi mwaka 2020 kesi ilipoanza.
“Baada ya mimi kushinda kesi akawa anawadanganya watu kwamba nitalipwa Sh. 50,000,000 ili niondoke hapa kwamba sijashinda… watu wakaendelea kuleta fujo nimepambana nao nikaenda TAA kuonana na Mkurugenzi hakutaka kuongea na mimi akanidampo kwa mwingine mdogo wakati jambo linamuhusu yeye” alisema
MGOGORO ULIVYOANZA
Februali 7, mwaka huu katika mitandao ya kijamii, walionekana wakazi wa eneo hilo wakilalamikia kitendo cha Elizabeth kufukua makaburi na kuchukua mabaki ya miili na kwenda kuitupa ili kupata eneo la kuwauzia watu.
Elizabeth Nyondo ni miongoni mwa waliwasilisha lalamiko lake katika video hiyo kwamba mtoto wake na mumewe wamezikwa eneo hilo hivyo hapendezwi na kitendo cha makaburi hayo kutaka kufukuliwa na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati wapate haki yao.
Hali hiyo ilimlazimu mpogolo kufika eneo hilo na jopo la mofisa wake kwaajili ya utatuzi na hatua za kisheria.
HATUA ZA DC.
Akizungumza na mwandishi wa habri hii Mpogolo alisema wananchi hao wanapaswa kuendelea na huku hatua kadhaa za kisheria zikifuata kwa viongozi.
Alisema viongzoi wa serikali za mitaa waliokuwa wanashuhudia uuzwaji wa eneo katika makaburi hayo na waliokuwa anafukua mabaki ya miili watachukuliwa hatua za kisheria na Jeshi la Polisi kwa sababu hilo ni kosa la jinai.
“Kuhusu hukumu iliyotolewa na mahakama Mwanasheria Mkuu wa serikali, TAA, Mamlaka za Serikali ya Mitaa, wameshakata rufani dhidi ya hukumu iliyotolewa lakini saula la makaburi liko pekeyake hata hukumu imemtaka alipwe fidia na sio kufukua.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED