Kanisa Katoliki Tanzania limepoteza kiongozi wa kipekee, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyefariki dunia usiku wa Februari 19, 2026, akiwa na historia ndefu ya huduma, maarifa na uongozi.
Kardinali Pengo, aliyejulikana kwa 'photographic memory' na akili ya hali ya juu (extra intelligent), alichangia kwa kiasi kikubwa katika malezi, elimu na maendeleo ya Kanisa Katoliki nchini.
Wanafunzi wake wa zamani wanasema uwezo wake wa kiakili ulikuwa wa aina yake. Stephen Mwakangale, mmoja wa wanafunzi wa Seminari ya Kaengesa, alisema jana kuwa alimtangulia darasa moja, lakini kwa akili na kumbukumbu ya picha, Kardinali Pengo alikuwa akitofautiana na wengine.
"Mwaka 1961 nilihamia Seminari ya Kaengesa darasa la saba, Kardinali alikuwa darasa moja mbele yangu. Alikuwa mtu wa kawaida sana, lakini alikuwa ‘extra intelligent’ na kitu kingine, alikuwa na photographic memory. Akiona kitu, kinabaki. Hata kusoma kitu mara moja, kingebakia akikumbuka bila shida," alisema.
Uwezo huo wa kiakili uliwezesha Kardinali Pengo kushiriki kikamilifu katika kazi za kanisa, hata wakati shule zilipokuwa zimefungwa.
Mwakangale alibainisha kuwa wakati wa likizo, Pengo alipelekwa moja kwa moja kwa Askofu wa Sumbawanga, ambako aliweza kutumia akili yake kwa kina katika masuala ya ushauri na uhasibu wa kanisa.
"Kardinali Pengo alikuwa mpole, si mzungumzaji sana, lakini akili yake ya kufikiri na kuunda hoja ilikuwa ya kipekee. Alishika nafasi za juu darasani kila mwaka, mara nyingi akiwa wa kwanza au wa pili," Mwakangale aliongeza.
Baada ya kuhitimu Seminari ya Kaengesa mwaka 1965, Kardinali Pengo aliendelea na masomo yake katika Seminari ya Kipalapala, Tabora, ambako alijitahidi kuendeleza elimu yake na kujiandaa kwa majukumu ya uongozi wa kanisa.
Ujuzi na maarifa yake yalichangia pakubwa katika malezi ya upadri wa kizazi kipya na ukuaji wa Kanisa Katoliki nchini.
UWEZO KIAKILI
Kardinali Pengo alikuwa miongoni mwa wachache wanaojulikana kuwa na photographic memory, uwezo unaomruhusu kukumbuka picha, maandishi, namba na maelezo kwa usahihi wa ajabu.
Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa kumbukumbu hii hufanana na kupiga picha kwa akili, ikiruhusu mtu kusoma ukurasa mara moja na kuweza kukariri maelezo yote bila kuharibu.
Zaidi ya hiyo, alikuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutatua matatizo, hali inayomweka katika kundi la watu wenye akili ya hali ya juu (extra intelligent).
Aina hii ya watu mara nyingi huitwa 'genius' au 'high IQ person', na Kardinali Pengo alikuwa mfano wa kweli wa mtu wa aina hii. Uwezo wake huu wa kiakili haukumsaidia tu katika elimu bali pia katika utendaji wake wa kidini na kijamii.
Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 katika Kijiji cha Mwazye, Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa.
Alifanya vizuri katika masomo yake ya awali hadi kuingia seminari, ambako aliibua vipaji vya kipekee. Aliteuliwa kushika wadhifa wa juu wa Kanisa Februari 21, 1988, na hatimaye alitangazwa kuwa Kardinali wa Pili Tanzania Februari 21, 1998, na Papa John Paul II.
Alistaafu rasmi Agosti 15, 2019, lakini alibaki kikomo cha hekima na ushauri katika jamii na Kanisa hadi kufariki dunia Februari 19, 2026, akiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.
Kifo chake kimehuzunisha wengi, hususan waamini wa Kanisa Katoliki na wale waliokuwa wamemfahamu kwa karibu.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi, mwili wa Pengo utazikwa katika Kituo cha Hija Pugu, Jumamosi ijayo, Februari 28, 2026.
Huko ndiko familia, viongozi wa kanisa, viongozi wa dini nyingine na wananchi wanatarajiwa kushiriki kuaga mwili wa kiongozi huyu wa kipekee.
MCHANGO KWA KANISA
Kardinali Pengo aliendeleza Kanisa Katoliki katika maeneo ya mbali nchini, akisisitiza elimu, malezi, na mafunzo ya upadri.
Uwezo wake wa kiakili na kumbukumbu ya picha ulimwezesha kuunda mikakati madhubuti ya maendeleo ya kanisa, kuhimiza ushirikiano wa jamii na kukuza shughuli za kijamii kama elimu na huduma za afya.
Mbali na malezi ya kiroho, Kardinali Pengo alihamasisha ufundi, uhasibu na usimamizi wa rasilimali katika taasisi za kanisa, jambo lililosaidia kuimarisha usimamizi wa fedha na miradi ya maendeleo ya jamii.
Shule na seminari nyingi zinazoendelea nchini zimetunukiwa urithi wa hekima na mifumo aliyoweka kwa vizazi vijavyo.
Wanafunzi wake wa zamani, waalimu na waumini wanakiri mchango wake wa kipekee. Mwakangale anasema:
"Alikuwa mfano wa kielelezo wa elimu na akili ya kipekee. Alituongoza kwa mfano, akitufundisha jinsi ya kutumia akili na maarifa kwa njia sahihi, si tu kwa masuala ya kidini bali pia maisha ya kila siku."
Mchango wake umeonekana wazi katika seminari za vijana, malezi ya upadri na huduma za kijamii.
Kardinali Pengo hakufanya kazi yake peke yake. Alihamasisha ushirikiano kati ya familia, kanisa na jamii, jambo lililosaidia kukuza maadili na maendeleo endelevu.
Kardinali Pengo alikuwa kiongozi wa kipekee aliyejulikana kwa akili ya hali ya juu na kumbukumbu ya picha, mchango wake katika malezi ya upadri na Kanisa Katoliki hauwezi kupuuziwa.
Alitoa mfano wa kuzingatia elimu, maadili, utendaji wa kisiasa na kijamii kwa mlingano unaowezesha maendeleo ya kweli.
Kuwapo kwake kulikuwa mwanga wa maarifa na kiini cha hekima, akionyesha kwamba kiongozi bora ni yule anayejali elimu, malezi, jamii na mustakabali wa vizazi vijavyo.
Kifo chake ni pengo kubwa, lakini urithi wake wa elimu, maarifa na ushawishi wa kiroho utaendelea kuangaza vizazi vipya.
Kwa Kanisa Katoliki Tanzania na taifa kwa ujumla, Kardinali Pengo atabaki kuwa mfano wa kipekee wa uongozi, maarifa na hekima.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED