‎Mgogoro wa mirathi aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali wazua sintofahamu ‎ ‎

By Imani Nathaniel , Nipashe Jumapili
Published at 04:09 PM Feb 22 2026
Wakili Peter Madeleka.
Picha: Imani Nathaniel
Wakili Peter Madeleka.

‎Mgogoro wa mirathi unaohusu mali ya aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali, marehemu Ernest Ndati Marasa Mashimba, umeibua sintofahamu kufuatia madai ya ubadilishaji wa umiliki wa hati kinyume cha utaratibu wa kisheria. ‎ ‎

‎Marehemu Mashimba alifariki dunia Septemba 19, 2010 na kuacha mali ikiwemo Kiwanja Na. 9 chenye Hati Na. 58933 kilichopo Usino, Msasani jijini Dar es Salaam. Nyumba iliyopo kwenye kiwanja hicho ndiyo inayozua mvutano kati ya warithi na baadhi ya wadaiwa kuhusika katika mchakato wa umiliki.


‎Kwa mujibu wa Wakili Peter Madeleka, shauri la mirathi lilifungwa rasmi na Mahakama ya Kinondoni baada ya mali za marehemu kuorodheshwa na kugawiwa kwa warithi halali. Nyumba hiyo ilirithishwa kwa Neema Ernest na Suzana Mashimba.


‎Madeleka amesema kuwa mwaka 2021 umiliki wa mali hiyo ulihamishwa rasmi kutoka kwa wasimamizi wa mirathi kwenda kwa warithi hao wawili. 


‎Hata hivyo, anadai kuwa Oktoba 2023 msajili wa hati Dar es Salaam alibadilisha tena umiliki na kuurudisha kwa wasimamizi wa mirathi licha ya zoezi la mirathi kuwa limekamilika.


‎Katika sakata hilo, mtu anayetajwa kwa jina la Ali Lubeya Alphan anadaiwa kuomba kibali cha kubomoa nyumba hiyo katika Manispaa ya Kinondoni wakati akiwa mpangaji. Wakili Madeleka anadai kibali hicho kilitolewa kimakosa huku kesi ya mirathi ikiendelea.


‎“Mirathi ikishafungwa hakuna tena msimamizi wa mirathi. Wamiliki halali ni Suzana na Neema. Serikali inapaswa kuingilia kati kuhakikisha wanapata haki yao,” amesema Madeleka.


‎Aidha, Madeleka amewataka makamishna wa ardhi na Ofisi ya Msajili wa Hati kutenda haki ili kuondoa migogoro ya ardhi inayozidi kuongezeka jijini Dar es Salaam.


‎Kwa upande wake, Neema Mashimba ameomba Serikali iingilie kati akidai kuwa tangu kifo cha baba yao wamekuwa wakiishi kwa tabu wakisubiri haki yao itendeke.