Wanakijiji waomba msaada kukamilisha ujenzi wa ghala

By Elizabeth John , Nipashe Jumapili
Published at 03:08 PM Feb 22 2026
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Chama cha Mkombozi wa Umma (CHAUMMA), Sigrada Mligo, akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wakati alipokwenda kukabidhi mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kuhifadhi na kuu
Picha: Elizabeth John
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Chama cha Mkombozi wa Umma (CHAUMMA), Sigrada Mligo, akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wakati alipokwenda kukabidhi mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kuhifadhi na kuu

Wakazi wa Kijiji cha Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wamekwama kukamilisha ujenzi wa nyumba (ghala) la kuhifadhi na kuuzia mazao yao, hali iliyowalazimu kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali ili kufanikisha kukamilika kwa mradi huo.

Ombi hilo limetolewa mbele ya Mbunge wa Viti Maalum (CHAUMMA) Mkoa wa Njombe, Sigrada Mligo, wakati alipokuwa akikabidhi mifuko 50 ya saruji kwa wananchi wa kijiji hicho.

Baadhi ya wananchi, akiwamo Bernadino Mligo amesema ujenzi wa ghala hilo ulianzishwa na wakulima wanne wa matunda ya parachichi na apple kwa lengo la kuboresha uhifadhi na masoko ya mazao yao. 

Hata hivyo, baadaye wakulima wengine waliungana nao na kufikia jumla ya wakulima 83.

Amesema hadi sasa wamefanikiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 27 katika ujenzi huo, lakini bado hawajaweza kuukamilisha kutokana na changamoto za kifedha.

Saruji ilitolewa kuunga mkono ujenzi
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada wa saruji, Sigrada amesema ghala hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwasaidia kuuza mazao yao kwa urahisi na kuongeza kipato chao.

Aidha, amewahimiza wananchi kuacha siasa na kuzingatia zaidi shughuli za maendeleo, huku akiahidi kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.

“Tuendelee kushirikiana katika jambo lolote la maendeleo na kuendelea kufanya kazi. Nina wadau ninaowaamini na nitakwenda kuwashirikisha ili tukamilishe ujenzi huu,” amesema Sigrada.