Kituo cha kupooza umeme cha Ziba wilayani Igunga mkoani Tabora kinatarajiwa kumaliza kabisa adha ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikiathiri vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo, hatua inayotajwa kuwa mkombozi mkubwa wa maendeleo ya wananchi.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 5.8 kutoka mapato ya ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akieleza kuwa ni kielelezo cha dhamira ya serikali kuboresha huduma za umeme nchini.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia endapo hitilafu itatokea katika eneo moja, maeneo mengine ya Igunga yataendelea kupata umeme bila kuathirika, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo tatizo sehemu moja lilisababisha wilaya nzima kukosa huduma.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa laini tano za matoleo ya umeme, miundombinu ya kusambaza na kudhibiti mifumo ya umeme, ofisi ya mitambo pamoja na kibanda cha walinzi na uzio wa kituo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu hiyo.
Kihongosi amesema miradi ya aina hiyo pia inaendelea katika maeneo ya Sikonge na Urambo ikiwa ni mkakati wa kuimarisha miundombinu ya umeme chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na suluhisho la haraka panapotokea changamoto.
Katika ziara hiyo, alikagua pia ujenzi wa Shule ya awali na Msingi Ibologero unaogharimu zaidi ya Sh. milioni 342 na kuwataka wananchi kulinda miundombinu ya maendeleo pamoja na kudumisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila ushirikiano kati ya wananchi, serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED