Nondo amjibu Kiliba kuhusu bilioni 200 Samia kwa vijana

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:50 PM Feb 15 2026
Nondo amjibu Kiliba kuhusu bilioni 200 Samia kwa vijana
PICHA: Mpigapicha wetu
Nondo amjibu Kiliba kuhusu bilioni 200 Samia kwa vijana

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo Abdul Nondo ameshauri usimamizi madhubuti, uwazi na miongozo sahihi katika utoaji wa fedha zilizotengwa na serikali ya awamu ya sita kwaajili ya uwezeshaji wananchi kiuchumi hususani kwa Vijana wa kitanzania.

Nondo amebainisha hayo katika andiko lake alilolitoa siku moja baada ya kuona mtandaoni chapisho la Geofrey Kiliba aliyekuwa akizungumzia siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika andiko lake ametahadharisha  uwezekano wa kuibiwa kwa fedha hizo, ikiwemo Sh bilioni 200 za Vijana iwapo kutakosekana utashi katika kusimamia mtiririko na ugawaji wake.

"Mwaka 2022 Waziri Mkuu wakati huo alisema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana ambao hutengewa Sh. Bilioni moja kila Mwaka, 2021 hadi Februari 2022 maombi ya Vijana yaliyokidhi vigezo kupewa mkopo katika hiyo Bil.1 ni maombi yenye thamani ya Mil.200, asilimia 20.5% tuu, huku takribani Sh. Milioni 795 zikiwa zimebaki bila kuwafikia walengwa. 

Hapo nondo alihoji...Kwamba fedha ilibaki sababu ya kukosa walengwa? kwamba vijana hawana Sifa ndio maana ilibaki? na ilivyobaki hiyo fedha ilienda wapi?"

"Mnatoa fedha bila kuziwekea muongozo wala taratibu. Mnategemea nini? Ni upi muongozo wa utolewaji wa hizo fedha kwa vijana? Nani anajua? Guideline ni ipi ili nijue taratibu za utolewaji wa hizo fedha, nijue Sifa na vigezo, nijue nafuata taratibu zipi, hakuna muongozo, kanuni wala Sheria zinazoongoza utolewaji wa fedha kwa vijana. Mnatengeneza mianya ya watu kuiba huku Vijana wakitajwa kutokuwa na sifa." Amesema Nondo.

Katika ahadi zake, CCM aliyekuwa Mgombea Urais Dk. Samia katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 pamoja na fedha hizo zilizoahidiwa, Ilani iliahidi pia kuhuisha mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuongeza upatikanaji wa mitaji na uelewa wa fursa za mikopo, kurahisisha ufikiwaji wa fursa hizo hususani kwa wananchi wa Vijijini ambapo wanufaika wanatajwa kuwa chini ya asilimia 28.2 kulinganisha na wanufaika wa Mijini.