'Kung'oa jino ni hatua ya mwisho'

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:53 PM Feb 22 2026
Kinywa
Picha: Mtandao
Kinywa

Wito umetolewa kwa kila mtanzania kulinda afya ya kinywa na kutokubali kung’olewa hata kama linauma, bila kupewa sababu na mtaalamu eneo hilo.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, amesema hayo akizungumza na NipasheDigital, kuhusu afya ya kinywa ikiwa ni mwendelezo wa elimu kwa umma.

“Licha ya kwamba jino lako linalouma, bila kupewa sababu nzito na zenye mashiko za kitabibu, usikubali kung’olewa. Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba kwenye vituo na hospitali.

Madaktari na Matabibu wa Kinywa na Meno wamefundishwa vyuoni kutibu Meno na Magonjwa yote ya Kinywani mwa mwanadamu. 

Ukiona Daktari au Tabibu wa Kinywa na Meno anakimbilia kung’oa jino lako, muulize “wewe mwenzangu umesoma chuo gani? Ina maana huko chuoni kwenu mmefundishwa kung’oa tu meno na matibabu mengine ya jino hamjafundishwa.?” 

Kwa ufupi mtanzania usikubali kung’olewa jino lako linalouma bila kupewa sababu nzito na zenye mashiko za kitabibu. Serikali imewekeza katika Vifaa Tiba na Dawa za Kutibia Magonjwa ya Kinywa na Meno kuanzia ngazi ya Kituo cha Afya (Health Center), Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufani za Mikoa, Hospitali za Rufani za Kanda, Hospitali, Maalumu na Hospitali ya Taifa.”