Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, amewaonya wakandarasi kujenga miradi chini ya kiwango.
Ametoa onyo hilo leo, Februari 22, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara.
Amesema, kwenye jimbo hilo hataki kuona miradi ya maendeleo ikijengwa chini ya kiwango na kwamba wakandarasi ambao wataendelea kutekeleza miradi ya namna hiyo, hato sita kuwachukulia hatua.
“kwenye jimbo langu sitaki kuona miradi ikijengwa chini ya kiwango, unakuta mkandarasi anaendelea na ujenzi wa barabara kiwango cha lami, lakini huku nyuma alipotoka barabara tayari ina mashimo kama vikaangio vya chapati, wakandarasi wa namna hiyo nitadili nao,” amesema Katambi.
Aidha, amemuonya pia Mkandarasi ambaye anajenga Stendi ya Mabasi ya kisasa, barabara ya kiwango cha lami kwenda hospitali ya Rufani ya Shinyanga, kwamba kama hana uwezo aachie kazi hiyo, kabla hajamchukulia hatua kali za kisheria, kutokana na kushindwa kuendana na kasi.
Aidha, amewasihi wakandarasi kwamba, pesa za miradi ya maendeleo ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali, wanapaswa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati kwa mujibu wa mikataba yao, na kwa ubora unaotakiwa na siyo kuchezea pesa hizo.
"Ukicheka na nyani, utavuna mabua, haiwezekani Rais anatoa pesa za miradi ya maendeleo, lakini wakandarasi wachache wanataka kuzichezea, kwa cheo changu nilichonacho cha Waziri wa Mambo ya Ndani, mtaipata freshi," ameongeza Katambi.
Katambi pia amewaonya watumishi wazembe na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa au kuonea wananchi, akiwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi, kwani serikali inasisitiza haki na usawa kwa wote.
Amewataka pia wananchi wa Shinyanga na taifa kwa ujumla, kuendelea kudumisha amani ya nchi, kwa kufuata Katiba, sheria na miongozo, ili amani iendelee kutawala.
Amewahidi wananchi, ataendelea kuwaletea maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, maji, afya, elimu na kuendelea kuleta vyuo vikuu na kuboresha vilivyopo.
Katambi, amemshukuru pia Rais Samia kwa kuendelea kumwamini na hata kumteuwa tena kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kwamba ataitendea haki nafasi hiyo katika kuwatumikia watanzania.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amempongeza na kumtaka kulishughulikia suala la vitambulisho vya NIDA kwa kusogeza huduma za usajili katika ngazi ya kata.
Amesema wananchi wengi wanakumbwa na changamoto ya kufuata huduma hizo wilayani, hali inayowalazimu kutumia gharama kubwa za usafiri.
Nao baadhi ya wananchi wamempongeza kwa kuitisha mkutano huo wa shukrani, huku wakiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED