DC, bodaboda walioandamana na kufunga barabara wakaa mezani

By Remmy Moka , Nipashe Jumapili
Published at 08:22 AM Jan 12 2025
Mkuu wa wilaya KIgoma Dk. Rashid Chuachua akiwa katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za madereva pikipiki Kigoma.
Picha:Mtandao
Mkuu wa wilaya KIgoma Dk. Rashid Chuachua akiwa katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za madereva pikipiki Kigoma.

BAADA ya maandamano ya waendesha bodaboda na bajaji mkoani Kigoma kutikisa huku wengi wao wakitiwa mikononi mwa polisi, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua, amewaita kusikiliza kero zao huku akiwataka kufuata taratibu zote za kisheria.

Akizungumza na madereva hao, Dk. Chuachua alisema serikali na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hawakuridhishwa na vurugu hizo. 

Alisema vurugu hizo za waendesha bodaboda na bajaji kufunga barabara  hawategemei kuona tena zikijitokeza kwa kuwa hazileti taswira nzuri kwa mkoa na taifa kwa ujumla. 

Dk. Chuachua alisema tayari wamefanya mazungumzo na viongozi wao wa vituo vya bodaboda ili kuhakikisha wanaweka mazingira ya hali ya utulivu baina ya wasafirishaji wa vyombo vya moto na serikali.

 Kadhalika, aliwataka madereva hao kuhakikisha wanafanya mchakato wakupata leseni ili kuondoa malalamiko yasiyo ya msingi pamoja na kutii sheria bila shuruti kwa kuwa serikali imepokea malalamiko yao na imeahidi kuyafanyia kazi. 

"Kuhakikisha mnakidhi matakwa ya vyombo vya usalama barabarani. Hakikisheni  mnaenda katika vyuo vya mafunzo ya udereva VETA ili muwe na uhalali wa kupata leseni na kuacha mivutano na Jeshi la Polisi,"  alisema. 

 Dk. Chuachua alisema ni vyema wakafanya shughuli zao kwa usalama zaidi ili kulinda uhai wao pamoja na watumiaji wengine wa barabara. 

Alisema kwa kipindi cha 2023 ajali za pikipiki zilitokea 42 huku waendesha bodaboda waliofariki ni 12 na watembea kwa miguu 17 huku 2024 zikitokea ajali 50 za bodaboda wakifariki Dunia, waendesha bodaboda 22 na watembea kwa miguu 16.

 Nao baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji, walisema wamepokea maelekezo hayo lakini wakiliomba Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa na utaratibu mzuri wa ukamataji kwa waendesha vyombo vya moto ili kuondoa migogoro baina yao pamoja na  sintofahamu hasa wanapokuwa wakikamata huku wamevalia kiraia 

Mmoja wa waendesha bodaboda hao, Ramadhani Musa, alisema wanategemea serikali itahakikisha wanawawekea hali nzuri ya shughuli zao na watatii sheria bila shuruti ikiwamo kwa wale ambao hawana leseni watafanya utaratibu wa kupata leseni za udereva.