TLS yaingilia kati sakata kukamatwa Dk. Slaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:12 AM Jan 12 2025
Rais wa Chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi.

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimevitaka vyombo vya dola kutofautisha kati ya majibizano ya kisiasa na makosa ya kijinai ili kutenda haki kwa watuhumiwa.

Rais wa Chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi, amesema kesho atakwenda kumwakilisha Balozi na Katibu Mkuu Mstaafu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Dk. Slaa alikamatwa na Polisi juzi asubuhi na saa 8:00 mchana alipandishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X jana, Wakili Mwabukusi alisema tuhuma zinazotokana na masuala ya kisiasa ni vyema zikashughulikiwa kwa misingi ya kisiasa, badala ya kuzihamishia kwenye mfumo wa jinai.

Alisema mfumo wa haki jinai haupaswi kutumika kama chombo cha visasi, kukomoa, au kunyima watu haki zao za kikatiba bali msingi wa kuwarekebisha wahalifu kwa haki na uwazi.

“Katika mazingira ya ukosoaji wa kisiasa, ni muhimu kuweka mipaka kati ya haki za kibinafsi na makosa ya jinai,” alisema.

Alisema mambo ya kibinafsi yashughulikiwe kwa njia za kibinafsi na si kwa kutumia nguvu ya dola isivyo halali.

“Tutaimarisha na kulinda utawala wa sheria kwa kujitokeza mahakamani mara zote, bila woga, tukisimama kidete kwa ajili ya ukweli, katiba, na sheria,” alisema.

Mwabukusi alisema matokeo ya kesi si jambo kuu, kilicho cha msingi ni kulinda misingi ya haki na kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa uadilifu.

ILIVYOKUWA MAHAKAMANI

Akimsomea Dk Slaa Shtaka, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki , Wakili wa Serikali, Clemence alidai kuwa  mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 9, mwaka huu, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikielezwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai.

Alidai kuwa aliandika ujumbe uliosomeka: "Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya... na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake."

Alidai kuwa mtuhumiwa katenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya Mwaka 2015.

Mawakili  wa utetezi waliofika mahakamani hapo juzi wakiongozwa na Peter Madeleka walieleza kushangazwa na kitendo cha mawakili wa serikali kutoa kiapo cha kupinga Dk. Slaa kupewa dhamana bila kuwashirikisha na kukubaliana kwa pamoja.

Akizungumzia suala hilo, Wakili Madeleka alisema dhamana ni haki ya mtu huwezi mnyima mtu kwa kuwa alitoa kauli ya jumla, kwa kuwa sheria ni uwanja unaohitaji uandilifu tofauti na walivyofanya mawakili wa serikali.

“Kiapo hicho kilikuwa hakijawasilishwa kwa mawakili wa upande wa pili (utetezi) lakini pia wameeleza kuwa kwa kuwa upelelezi haujakamilika wameomba iahirishwe na ndugu Slaa asipewe dhamana kwa sababu ya usalama wake,” alisema 

Madeleka alisema  walipopata taarifa za kukamatwa kwa Dk. Slaa  juzi asubuhi  walifuatilia katika vituo vya Polisi vya Mbweni, Osterbay na Kituo Kikuu bila mafanikio.

Alisema baadaye walikutana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, aliyewaeleza makosa yanayomkabili na kuwa alipelekwa katika Mahakama ya Kisutu.