SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amewahimiza mama na babalishe, kupika vyakula kwa kutumia nishati safi, ili kulinda afya zao, kutunza mazingira kwa manufaa ya kijamiina kiuchumi.
Tulia, aliyasema hayo akihitimisha Tamasha la Mashindano ya Mapishi ya Vyakula kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia (Tulia Cooking Festival) lililofanyika, mwishoni mwa wiki jijini Mbeya.
“Lengo la kuandaa tamasha hili ni kuongeza uhamasishaji kwa jamii kuhusu elimu na matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na wote tunafahamu kwamba ajenda hii imebebwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika na sasa ametambuliwa pia duniani kwa ujumla,” alisema Dk. Tulia
Alieleza kwamba tamasha hilo limehusisha Mamalishe na Babalishe 1,000 akiwapongeza kwa kutumia jukwaa hilo, ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo, akisema taasisi mbalimbali nchini kuandaa matamasha kama hayo kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Pia Dk. Tulia, aliwapongeza wadau wa maendeleo kwa kudhamini Tamasha la Tulia Cooking Festival’ akiwamo kampuni ya gesi ya ORYX, Cocacola, EWURA na wadau wengine.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema serikali imeandaa mkakati wa matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, ili kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifakapo mwaka 2034.
“Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kutoa mitungi ya gesi ambapo mwaka 2023 serikali ilitoa zaidi ya mitungi 104,000 na mwaka huu inategemea kutoa mitungi 450,000,” alisema Kapinga.
Aliongeza kwamba nishati safi za kupikia zipo za aina nyingi ikiwemo gesi, umeme, majiko banifu na majiko mengine, pia alisisitiza kuwa nishati safi ni bora kwa kuandaa chakula kuliko nishati nyingine kama kuni na mkaa.
Kuhusu kupunguza bei ya gesi, alisema serikali inaendelea na mikakati ya kuwasaidia watu wengi kutumia nishati hiyo kwa gharama nafuu na alizitaka kampuni za gesi kuendelea kufanya ubunifu, ili kuhakikisha wananchi wananunua gesi kwa kiasi cha fedha walichonacho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED