MWENYEKITI wa Wazazi (CCM), Mkoa wa Morogoro, ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule ya Msingi na Awali East Africa ya jijini Dodoma, Dk. Rose Rwakatare, ameipongeza serikali kwa kuanzisha mitaala mipya ambayo amesema itasaidia watoto kujifunza kwa vitendo
Dk. Rose amesema lengo lao ni kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu ili kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha elimu na kuongeza ufaulu kwa mkoa huo wa Dodoma.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya pili ya darasa la saba shule ya msingi na awali ya East Africa Dodoma.
"Tunaishukuru sana serikali kwa kuanzisha mitaala mipya ambayo itakwenda kusaidia watoto wetu kujifunza kwa vitendo na sisi tunaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuupandisha chati mkoa huu kielimu"alisema
Dk.Rose Alisema shule hiyo imekuwa ya tatu kimkoa katika matomeo ya mtihani wa moko mwaka huu na kuongeza kuwa katika darasa la saba mwaka huu jumla ya watoto 70 watafanya mtihani na kwa namna walivyo waandaa wanatarajia kuwa na ufaulu wa juu katika mitihani wa taifa.
Alisema shule hiyo ilianza na wanafunzi 30 lakini kutoka na ubora wa elimu wana wanawanafunzi zaidi ya 900 na kwamba hivi sasa wamekamilisha ujenzi wa shuke ya sekondari ambayo itaanza mwakani lengo likiwa ni kutoa huduma bora ya elimu kwanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.
Hata hivyo, aliwataka wazazi ambao wamekuwa na tabia ya kushawishi watoto wa kike kufanya vibaya kwenye mitihani ya darasa la saba ili waolewe kuacha tabia hiyo kwakuwa huo ni ukatili.
"Mimi nikiwa kama mdau wa elimu nchini suala hili la wazazi kuozesha watoto waliomaliza darasa la saba ni kuwanyima haki yao ya msingi na ni kosa kisheria hivyo wawaache watoto hawa wapate haki yao ya msingi"alisema
Naye Kaimu Ofisa elimu mkoa wa Dodoma Prisca Myala, ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ulawiti pamoja na vitendo vingine vya ukatili kwa watoto wa kiume nchini wazazi wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuzungumza na watoto wao muda wote ili kujua changamoto wanazopitia wakiwa shule na nyumbani.
Myala, alisema kutokana na ongezeko kubwa la matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto wa kiume wazazi wanapaswa kuongeza ukaribu na watoto wao ili kujua madhira wanayopitia wakiwa shule, njiani na hata nyumbani.
“Wazazi lazima muweke utaratibu wa kuzungumza na watoto wakati mwingine watoto wanataka kutushirikisha changamoto zao lakini hatuwapi nafasi ya kujua nini wanakabiliana nacho wakiwa shule,njiani ama nyumbani"alisema
Alisema, wazazi wengi wamekuwa hawana muda wa kuzungumza na watoto wao kutokana na kutumia muda mwingi kwenye utafutaji wa riziki.
"Akinamama tusisahau jukumu letu la asili la malezi kwa watoto wetu akina baba wako bize na utafutaji wa maisha hata kama ni hamsini kwa hamsini lakini hatupaswi kusahau jukumu letu la asili la kulea watoto na kuwapa ulinzi"alisema
Aidha, alisema kutokana na mmomonyoko wa maadili hivi sasa katika jamii hakuna mtu wa kumwani kwa watoto hata kama ni ndugu wa karibu.
“Hata ndugu siyo watu wa kuwaamini kabisa kuna ndugu wa karibu ambao wanalawiti watoto hivyo hakuna mtu wa kumwamini kwa mtoto wako kama unataka mtoto wako awe vile unavyotaka hauna budi kumlinda dunia ya sasa siyo kama ile ya zamani mambo yamebadilika sana"alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED