NI lugha gongana. Ndivyo inavyoweza kuelezwa kutokana na sheria za nchi katika suala zima la umri wa kijana kuanza kutumia kilevi kama pombe na sigara.
Sheria za Tanzania zinaruhusu mtu mwenye umri kuanzia miaka 15 kuanza matumizi ya pombe, lakini wazalishaji wa bidhaa viwandani wameweka masharti kwamba: “Hairuhusiwi kutumiwa na kijana chini ya miaka 18.”
Kukiwa na rukhsa hiyo ya kisheria (Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe ya Tanzania ya Mwaka 1968) kwamba bidhaa hiyo inaweza kuuzwa kwa watu wenye umri wa kuanzia rika hilo, Sheria ya Ulinzi wa Mtoto ya Mwaka 2009 inaelekeza wazazi na walezi kuwalinda watoto dhidi ya tabia hatarishi, ikiwamo na unywaji wa pombe.
Wakati sheria zikielekeza pombe iuzwe katika maeneo maalum na kuwa na umbali wa kilomita moja kutoka baa moja kwenda nyingine, pia kukiwa na maelekezo ya muda maalum kuuza kilevi hicho, kinachoshuhudiwa mtaani hivi sasa ni lugha gongana kati ya pombe na sheria.
Mratibu wa Kinga ya Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Goodluck Tumaini, anasema Tanzania ina sheria ya zamani ya pombe, hivyo serikali inaendelea kuifanyia utaratibu.
“Tuna Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe ya Tanzania ya Mwaka 1968. Ukisoma sheria ile imeweka leseni mbalimbali. Leseni namba moja ni ya kioski, namba mbili ya maduka ya kawaida, namba tatu ni ya baa, namba nne ni ya klabu na namba tano inahusu hoteli. Sheria inasimamiwa na halmashauri,” anasema.
Anasema sheria hiyo inaruhusu mtu kuanza matumizi ya pombe kuanzia umri wa miaka 15 na zaidi.
“Kwa Tanzania tuna wanywaji wachache wanaokunywa pombe lakini wanakunywa sana lita 10.4. Hiki ni kiwango kikubwa sana cha pombe lakini kuanzia umri wa miaka 15. Kwa hiyo, ukimkuta kijana wako wa miaka 15 anakunywa, usianze kupambana naye, tuna wajibu wa kutoa elimu.
“Lakini sheria inasema usiuze pombe kabla ya muda wa saa 10, lakini leo hii kuna baa zipo kama hospitali watu wanaingia shift (zamu) nne, haijawahi kufungwa kaunta,” anasema.
“Hata kama sheria ni ya mwaka 1968, lakini imekataza. Sheria imekataza kuchanganya unga, sukari, juisi na pombe. Leo hii kuna vioski vya ‘Kwa Mangi’ watu wengi wanakaa pale.
Kadhalika, anasema sheria inamtaka anayefungua baa, asiweke muziki wa kuvutia watu na duka la pombe kati ya duka moja na lingine liwe kilometa moja.
“Leo hii kuna baadhi ya mitaa ukienda nyumba, baa, nyumba, baa, nyumba, baa. Hata kama ulikuwa huna mpango wa kunywa utakunywa tu. Sheria hiyo hiyo inakutaka nje ya wewe, usiweke mziki, lakini mtoto asipite katika eneo la pombe, leo hii ukienda katika baa unakuta watu wapo bwaaa.
“Sheria hii imeruhusu unywe pombe asubuhi kwenye leseni namba tano ya hoteli peke yake, lakini ukinywea kwenye hoteli uende ukanunue uingie chumbani ujifungie unywe pombe yako na ukimbughuzi yeyote yule umevunja sheria,” anasema.
POMBE DAWA YA KULEVYA
Tumaini anasema upatikanaji wa pombe umekuwa rahisi ndani ya nchi na kusisitiza kuwa kuwa pombe ni dawa za kulevya kama dawa nyingine na tumbaku zote zinasababisha ugonjwa unaoitwa uraibu.
“Uraibu ni ugonjwa kama magonjwa mengine. Ugonjwa sugu wa ubongo unaojirudia rudia unaosababisha mtu kupoteza thamani yake ndani ya jamii. Akianza kuwa na uraibu, atauza vitu ili tu akanunue pombe au tumbaku au dawa za kulevya,” anasema.
Hata hivyo, Tumaini anakumbusha kuwa huduma za matibabu zipo na wataalam wote wamejengewa uwezo.
Kuhusu sigara na pombe anasema zote zina madhara yake na kila moja ina sheria.
“Sigara ina Sheria Namba 121 ya Mwaka 2003 ya kudhibiti matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kanuni zake za mwaka 2014. Sheria hii ukisoma Kifungu cha 24 hadi 29 inazungumza masuala ya udhibiti wa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kuwataka wanaouza kuweka maeneo maalum,” anasema.
Tumaini anasema ni muhimu kuendelea kuhimiza anayekaa karibu yako na kuvuta tumbaku anafanya kosa la kisheria.
SHISHA, SIGARA BALAA
Anasema changamoto kubwa iliyoko katika bidhaa hizo, wakati ambao sasa kuna shisha na sigara za kieletroniki, imekuwa ni ngumu kwa mzazi au mlezi kugundua kama mtoto wake anavuta, kwa sababu nyingine zimetengenezwa kama kalamu.
“Changamoto nyingine ni matumizi ya shisha yaliyopitiliza, huku sheria yetu haijazungumza masuala ya shisha. Changamoto kubwa inayotokea sasa ni pamoja na kuchanganya dawa za kulevya katika shisha.
“Unaweza kukaa na anayevuta shisha, wewe unakunywa bia zako, ukifika nyumbani hata mlango wa choo hukumbuki, umevutishwa,” anasema.
Tumaini anawataka waandishi wa habari wakafanye habari za uchunguzi kuhusu mambo hayo na kuelimisha umma kuhusu matumizi ya bidhaa za tumbaku zikiwamo shisha, sigara za kieletroniki na pombe kwa kuonesha hatari iliyoko mbele yao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk. Omari Ubuguyu, anasema matumizi ya tumbaku yamepungua kwa sasa kulinganisha na huko nyuma.
“Matumizi ya sigara yamekwenda chini katika watu wenye umri mdogo. Lakini katika kundi la vijana umri wa miaka 18 kuendelea wanatumia katika mtindo wa shisha na bahati mbaya wanatumia sigara nyingi zaidi kwa kutumia shisha ambazo zimewekewa ladha tofauti,” alisema.
“Matumizi ya pombe yamevuka kiwango Tanzania. Takwimu za dunia kiwango cha utumiaji wa pombe Tanzania kinazidi kiwango cha utumiaji wa pombe Urusi.
“Takwimu za sasa zinaonesha matumizi ya kiwango cha pombe kinachotumika Tanzania kinazidi cha Russia. Kama utachukua pombe yote inayotumika na kugawanya kwa raia wote watu wa miaka 15 na zaidi. Watu wenye umri mkubwa zaidi Urusi (Russia) ni wengi zaidi kuliko huku kwetu. Sisi watu wenye umri mdogo miaka sifuri hadi 14 wanakaribia asilimia 40 ya watu wote.
“Kwa hiyo wenye umri mdogo ni wengi. Nikichukua miaka 15 kuendelea ukagawia pombe inayotumika Tanzania, kila mtu anakuwa na ndoo ndogo ya pombe nyumbani kwake, na kuwa ndiyo kiwango cha matumizi ya pombe kwa mwaka. Tunamaanisha pombe ambayo ni asilimia 100 ukichanganya unaweza kutengeneza pipa la bia,” anasema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Prof. Andrew Swai, anasema Tanzania imekuwa nchi ya tatu Afrika kwa unywaji wa pombe.
“Huko nyuma tulikuwa tunazungumzia Zambia ni walevi, sisi sasa tumekuwa zaidi. Kwa hiyo, pombe siyo nzuri inaharibu ubongo, ini na figo na kumfanya mtu kushindwa kufanya kazi vizuri, inasababisha ajali za barabarani,” anasema.
MADHARA YA POMBE
Magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa yanatajwa kuwa tishio nchini, unywaji pombe kupitiliza na na uvutaji sigara na vileo vingine jamii ya tumbaku vikiwa sehemu ya visababishi vikuu vya maradhi hayo.
Madhalani, kwa ugonjwa wa figo pekee, Tanzania ina wagonjwa karibu 3,000 ambao wana matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi na kila mwaka serikali hutumia Sh. bilioni 56 mpaka Sh. bilioni 80, kwa ajili ya kununua vitendanishi ili kuwahudumia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED