SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema timu yake ya Taifa Stars sasa imekuwa na uchu wa kushiriki kila fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambazo hufanyika kila baada ya miaka miwili, imeelezwa.
Taifa Stars inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuikaribisha Ethiopia katika mechi ya Kundi H ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Baada ya mechi hiyo Stars itasafiri kuelekea Guinea kwa ajili ya mchezo mwingine wa kundi hilo utakaochezwa Septemba 10, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, aliliambia gazeti hili jana maandalizi yanaenda vizuri na anaamini Taifa Stars itapata tena tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Ndimbo alisema kufanya vizuri kwa mchezo dhidi ya Ethiopia itatusaidia kupiga hatua kuelekea kufikia malengo ya kufuzu.
"Tumeanza kunogewa kwa kufanya vizuri kwa timu zetu za taifa, kwa wanawake, wanaume na michuano mbalimbali, ...kaka zao kina Adolph alicheza, tukaja kufuzu baada ya miaka 39, lakini tukacheza tena hizi zilizopita, tumepunguza muda," alisema Ndimbo.
Aliongeza kutopata tiketi ya kufuzu fainali za mwakani itakuwa ni 'deni' kwa timu yetu ambayo itakuwa mwenyeji kwenye fainali za mwaka 2027.
"Matokeo mazuri yatakuwa nguvu ya kufanya vizuri katika mechi ya pili ya ugenini, ingawa haikatazwi kupata ushindi ugenini, ukifanya vizuri kuanzia mwanzo unajipunguzia mlima, wachezaji wanajua hilo, benchi la ufundi wanatambua hilo, mdau namba moja kwa maana ya serikali anatambua hilo," Ndimbo alisema.
Aliongeza kwa kuwaita mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kufanikisha Stars inaanza vyema kampeni zake.
Naye Kiungo wa Stars, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema wako tayari kwa ajili ya mechi hizo mbili na wanawaomba mashabiki wajitokeze kuwashangilia keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED