Apoteza maisha akiogelea wakati wa Krismasi

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 02:10 PM Dec 29 2024
Mwogeleaji
Picha: AI
Mwogeleaji

MKAZI wa Mtaa wa Bukondamoyo, Kata ya Mhungula, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Mbaraka Magese (24), amekutwa amefariki dunia akiwa kwenye bwawa la kuogelea siku ya Sikukuu ya Krismasi.

Mwili wa marehemu ulikutwa ukielea katika bwawa hilo lililoko katika baa ya Nzengo Grill, Mtaa wa Mbulu, kata ya Mhongolo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi,  alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa mpaka sasa wanamshikilia msimamizi wa bwawa hilo kwa uchunguzi zaidi.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini Magese alifariki dunia akiwa anaogelea huku mvua inanyesha na alizidiwa baada ya kunywa maji mengi.

Aidha,    Magomi aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe pamoja na maeneo ya kuogelea kuwa waangalifu pia kufunga mabwawa ya kuogelea wakati mvua ikinyesha ili kuepusha madhara kama hayo.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Stanley Luhwago, alisema wasimamizi wa mabwawa hayo lazima wawe na ujuzi wa kuogelea pamoja na vifaa vya kuogelea kama majaketi na maboya ili kuhakikisha usalama kwa waogeleaji kwa kuwa wako wengine hawajui kuogelea kabisa na michezo hiyo wanaitamani.

Alisema ili kuondoa majanga hayo kuendelea kutokea, wamejipanga kuwatembelea wamiliki wa mabwawa hayo pamoja na wasimamizi wao kuwapatia elimu ya kuwakinga na majanga wateja wao na kuhakikisha hakuna uogeleaji unaweza kufanyika wakati wa mvua.

“Ni ngumu kumtambua mtu asiyejua kuogelea kwenye mabwawa haya lakini ni rahisi kudhibiti majanga haya yasitokee kwa sababu msimamizi alipaswa kumzuia marehemu kuogelea kutokana na mvua iliyokuwa inanyesha siku hiyo.

“Tuendelee kuzingatia matakwa ya kisheria tunayowapatia kabla ya kujenga mabwawa haya," alisema Luhwago.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameagiza baa hiyo ifungwe kutokana na kutokidhi vigezo vya usalama katika huduma za kuogelea na upelelezi ukikamilika na kubainika kuna uzembe ulitendeka, mmiliki wake achukuliwe hatua za kisheria.

Alisema wamiliki wa mabwawa ya kuogelea wanapaswa kuzingatia sheria na kanuni zinazohusiana na uendeshaji wa mabwawa ili kuepuka majanga kama hayo na wale watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa mabwawa hayo kuendelea kufanya kazi.