MATUKIO ya kupotea na utekaji wa watu maeneo mbalimbali nchini, yamewaibua wazee wa mila, machifu na waganga wa jadi na kueleza kuwa kinachofanyika ni udhalilishaji wa utu na kuliletea taifa sifa mbaya.
Makundi hayo ya watu yameibuka baada ya mapema wiki hii, Jeshi la Polisi kutangaza kuwashikilia watu kadhaa, akiwamo mganga wa kienyeji, huku miili ya watu 10 ikifukuliwa mikoa tofauti nchini baada ya kudaiwa kuuawa na watuhumiwa hao.
Baadhi ya miili hiyo ilikutwa imezikwa kwa mfumo wa kukaa na wapo watoto wa watuhumiwa akiwamo mtoto wa mganga huyo wa kienyeji ambao walizikwa hai katika zizi.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali, baadhi ya wazee wa kimila na waganga wa jadi, wameiomba serikali kufanya ufuatiliaji wa kina dhidi ya waganga wanaofanya ramli chonganishi na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mkoani Shinyanga, Salumu Zarua alisema: ““Kupotea kwa watoto na utekwaji wa watu ni kulidhalilisha taifa kwamba hakuna amani tena na vyombo vya ulinzi na usalama havipo. Sisi wazee tunaomba serikali iamke kudhibiti vitendo hivi.”
Mganga wa jadi, Elias Tungu, alisema matukio mengine ya kupotea kwa watoto yanahusiana na imani za kishirikina ambayo husababishwa na waganga wa kienyeji. Aliiomba serikali ifanye msako wa kuwabaini waganga ambao wanapiga ramli chonganishi na wale wasio na leseni.
Kutokana na kuwapo kwa matukio hayo, alitoa wito kwa wazazi kuwa makini na watoto wao kwa kufuatilia mienendo yao hasa wanakocheza na kuacha kuwatuma dukani nyakati za usiku.
“Katika mkoa wa Shinyanga kwa mwaka huu, tayari kuna matukio manne ambayo yamehusisha watoto kupotea, huku mmoja akipatikana akiwa ameuawa kwa kukatwa viungo vyake,” alisema.
UCHAGUZI SABABU?
Mkoani Mwanza wazee wa kimila walisema vitendo hivyo, vinatokana na watu wanaotumia kivuli cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Walisema vitendo hivyo vinatakiwa kukomeshwa haraka iwezekanavyo kwa kuwa kuendelea kwa matukio hayo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katibu wa Machifu Tanzania, Aron Mikomangwa, alisema uchaguzi wa serikali za mitaa hauwezi kusababisha ukatili huo, bali kuna watu wanatumia mwamvuli huo kuteka watoto.
“Mwenyekiti wa mtaa yeye anajitolea hana chochote cha kupata hadi akafanye utekaji wa watoto? Wako wanaofanya unyama huo, hususani wanasiasa wa uchaguzi mkuu, wafanyabiashara wa madini. Watu wanaotafuta utajiri na wanaouza viungo vya binadamu. Hao ndio wanaoshirikiana na waganga waovu kuchafua amani,” alisema.
Alisisitiza kuwa hakuna uganga unaoelekeza kuteka watoto au vitendo vya kihalifu, bali kuna waganga wasiyofuata maadili na wananchi wenye uchu wa utajiri na madaraka, wanafanya mambo hayo kwa matakwa yao kwa kukosa utu na hofu ya Mungu.
"Sisi machifu ndio walezi wa waganga. Tunatamka hatuungani na mganga yoyote anayetoa maelekezo ya wateja wao kufanya ukatili wowote, hivyo tunaiunga mkono serikali iwakamate na itoe adhabu kali kwa yeyote atakayeonekana amekwenda kinyume cha maadili,” alisema.
WAKAMATWE
Chifu wa Mkoa wa Dodoma, Mazengo wa Pili, aliitaka serikali kuendesha operesheni maalum ya kusaka waganga wasio na leseni na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mazengo alisema wakiwa viongozi wa kimila, wanalaani mauaji utekaji wa watu, vitendo ambavyo vinaendelea kujenga hofu miongoni mwa watanzania.
“Sisi umoja wa machifu Mkoa wa Dodoma, tunalaani vitendo hivi na tunaiomba serikali kuchukua hatua kwa waganga wa kienyeji ambao watabainika kuhusika katika matukio haya ya mauaji na utekaji," alisema.
Alisema kutokana na vitendo hivyo, wamechukua hatua za kukabiliana navyo kwa kuunda vikosi vya sungusungu ambapo kila baada ya nyumba kumi atakuwapo kiongozi.
“Hii itasaidia kila mgeni anayeingia katika maeneo yetu anajulikana anatoka wapi, kazi yake ni ipi, ili kukabiliana na vitendo vya utekaji na mauaji,” alisema.
Naye Katibu wa Umoja wa Machifu Dodoma, Ndahani Chinang'anang'a, alisema wanalaani vitendo hivyo kwa sababu hivi sasa jamii inaishi kwa hofu kubwa kutokana na matukio hayo.
Chinang’anang’a alisisitiza haja ya serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki ili kukomesha hali hiyo.
Chifu wa Ukoo wa Wahejiu wanaotokana na kabila la Warimi, Ikungi mkoani Singida, Thomas Mgonto (pichani), alisema matukio ya mauaji kutokana na imani za kishirikina hayakubaliki katika jamii yeyote ile.
“Sisi kama machifu hatukubaliani na matukio haya, tunapinga na tunalaani vitendo, hivyo kwani jamii yeyote ile hata kama haijastaarabika, hata kama haina elimu, hata kama haifahamu lolote utu wa mtu, uhai wa mtu ni jambo la muhimu sana katika ustawi wa himaya yeyote,” alisema.
Chifu Mgonto alisema wao kama viongozi wa kimila ifahamike kuwa hakuna mila yeyote katika jamii iwe ya Wanyaturu ambayo inaweza kukubaliana na vitendo vya mauaji ya watu, kwani mila zao zimenyooka.
Alisema ili kukomesha vitendo hivyo, serikaii na taasisi zote zisizo za kiserikali waendelee kukemea vitendo hivyo na wananchi wawe wanatoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kwa kutoa taarifa za watu wanaowahisi.
Pia alisema serikali na taasisi zisizokuwa za kiserikali, zisaidie kutoa elimu kwa wananchi, kuachana na imani potofu kwamba, kuua mtu na kuchukua viungo vya binadamu watapata utajiri.
"Watu wanaweza kusema haya yanayotokea ni mambo ya kimila hapana. Ni mambo ya watu binafsi ambao wanaingia katika mgongo wa kimila. Tunataka jamii yetu ielimishwe, ifahamu hasara ya kufanya vitendo hivyo ambavyo kimsingi, vinaharibu mila na desturi za kitanzania,” alisema.
Chifu wa Unyahati, Adamu Gwau, alisema kutokana na matukio hayo,machifu wa Mkoa wa Singida wamepanga kukutana kujadiliana na kuweka mikakati itakayosaidia kukomesha vitendo hivyo.
“Matukio haya yamedhihirisha ni jamii yetu ndio inahusika, hivyo sisi kama machifu tuwe wakali kukemea mambo haya,” alisema.
Mzee wa Mila Wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, Keya Kashu, alisema pamoja na kuwapo kwa matukio hayo kuna tetesi kwamba wanaohusika na kuwatoa watu viungo ni shinikizo la watu wanaonunua figo kutoka nje ya nchi.
Kashu alisema pamoja na kwamba, waganga wa kienyeji wanachangia kutokana na masharti kwa baadhi ya wagonjwa, lakini kipindi cha nyuma walikuwa wanahitaji zaidi viungo vya albino, lakini serikali imepigana na matukio hayo kupungua.
“Ni jambo linalopaswa kukemewa na ni uonevu, ukatili na unyama mkubwa unaotia hofu. Sisi wazee wa mila tunatetea kwa nafasi yetu, lakini serikali inapaswa ifike hadi ngazi za chini katika jamii kuongea na mwananchi mmoja mmoja ili kupata suluhu ya kudumu” alisema Kashu.
Alisema wako wananchi wanaojua wahusika wa matukio hayo katika ngazi za chini, lakini kwakuwa ushirikiano ni mdogo kutoka serikalini wanaamua kukaa chini.
Wazee wa kimila mkoani Tabora akiwamo Mohamedi Thabith (70) alisema, “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani, watu wameanza kujipanga kutafuta nafasi za uongozi na kuna watu nao wanatumia mwanya huo kujifanya ni waganga, ili wapate fedha wakati sio wataalamu. Ndiyo hawa wanatuleta mabalaa haya kwa kuwatuma watu wawaletee watoto ana viungo vyao.”
· IMEANDALIWA na Paul Mabeja (Dodoma), Marco Maduhu (Shinyanga), Rose Jacob, (Mwanza), Thobias Mwanakatwe (Singida), Benny Kingson (Tabora) na Halfan Chusi (Dar)
00000
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED