MABINGWA wa Ligi Kuu Zanzibar, JKU wanatarajia kukutana na Chipukizi kutoka Pemba katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Amaan Complex.
Mechi hiyo ni maalumu kwa ajili ya kufungua rasmi pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar 2024/2025.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Chipukizi, Mzee Ali, alisema wamejiandaa vyema kucheza soka la ushindani ili kuhakikisha wanabeba ngao hiyo.
Ali alisema ingawa mchezo huo sio rahisi kama unavyozaniwa lakini mipango yao mikubwa ipo kuhakikisha wanaanza msimu mpya kwa 'kishindo' kwa kucheza kwa tahadhari.
"Tumejiandaa kuhakikisha hatufanyi makosa kuelekea mchezo huu muhimu wa ufunguzi wa ligi yaani Ngao ya Jamii, tunaamini kesho (leo) ni kupata ushindi na kuipata ngao ili kuwa na hamasa zaidi kuelekea msimu mpya," kocha huyo alisema.
Naye Kocha wa JKU, Salum Haji, alisema licha ya kuwa na majeruhi watatu wa kikosi cha kwanza lakini anakikosi kipana kitakachotetea ngao hiyo.
"Tunashuka uwanjani kwenda kuitetea ngao yetu ambayo mwaka jana tuliichukua na mwaka huu lengo kushinda kwa idadi kubwa ya magoli," alitamba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED