Ajali yaua wanne, watatu wajeruhiwa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 09:29 AM Dec 15 2024
Ajali.
Picha: ITV
Ajali.

WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Hamis Mungwana, alisema tukio hilo lilitokea jana asubuhi katika Kijiji cha Unyampiti, Kata ya Unyahati, wilayani Ikungi, mkoani Singida.

Alisema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Alphard lenye namba za usajili T 128 EKF, mali ya Anastazia Gozbert, ambayo iligongana na lori lenye namba za usajiri T 467 EJP ikiwa na tela lake, T 439 EJN aina ya Howo, mali ya East Africa Logistic Ltd, ambayo lilikuwa likitokea Singida kwenda Dar es Salaam.

Mungwana alisema waliofariki dunia ni wanaume na majina yao hayajafahamika na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Singida (Mandewa).

Alisema kati ya majeruhi watatu, mmoja ametambuliwa ambaye ni Mauldi Mbalima, mfanyabiashara wa Korogwe Pwani ambaye amejeruhiwa miguu.

“Majeruhi wengine wawili wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 45 hali zao ni mbaya na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Singida,” alisema.

Kamanda Mungwana alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari aina ya Toyota Alphard kuendesha gari kwa kasi na kwenda upande wa pili na kugonga lori la mizigo.