MOJA ya swali unaloanza kujiuliza inapofika kila mwisho wa mwaka ni siri gani iliyojificha kwa kabila la Wachaga kuiteka nchi kwa shamrashamra zinazotokana na utamaduni wa kurudi kwao kuhiji wakiwa makumi kwa maelfu.
Watu wengi wanafikiria kwamba Wachaga wanatokana na asili moja. Ukweli ni kwamba wamegawanyika katika himaya 15, wanatofautiana kwa lafudhi, lugha, rangi na mwonekano wa miili yao.
Utamaduni wa Wachaga wa kufunga safari kila mwaka kurudi nyumbani msimu wa krismasi, umekuwa ukiwashangaza wengi na kuwaacha na maswali yasiyo na majibu.
Mzee Jossen Abel Moshi (87), Mkazi wa Mbokomu, Moshi mkoani Kilimanjaro, anasema utamaduni huo unajengwa na hoja kwamba huwa wanarejea makwao kila mwisho wa mwaka kwa ajili ya kupumzika na kujadili mambo yao.
“Wanakuja kupumzika baada ya kufanya kazi zao kuanzia Januari mpaka Desemba, wanarudi nyumbani kuungana na wenzao na hata wengine ambao hujawahi kuwaona kwa kipindi cha mwaka mzima, basi wanakuja nyumbani kusherehekea hiyo sikukuu na kupumzika,” anasema.
Alipoulizwa kama kweli wanakwenda kufanya matambiko. Mzee Moshi anasema: “Yale mambo ya kizamani ya kufanya matambiko yalishaisha kabisa; na kipindi kile watu walikuwa hawasafiri sana, walikuwa wanaishi tu nyumbani, wala hawakuwa wanatoka mbali.
“Isipokuwa mwisho wa mwaka, huwa wanakuja nyumbani wanachinja mbuzi, ng’ombe kwa ajili ya kusherehekea krismasi na mwaka mpya, kulingana na jinsi familia au ukoo wao walivyo wengi. Hili linategemea na uchumi wa kila familia au koo.
“Wanapokutana kula hicho chakula, huwa wanakutana kuongea mambo yao ya kifamilia, kukemea uvivu, ulevi na hata kusaidiana ndugu wanapokwama kiuchumi. Kimsingi huwa wanakemeana kwa wale wanaoonekana wanaenda kinyume na malengo ya familia.
Watoto wa kiume, walevi, kinababa wavivu, hivyo vikao kwao huwa ni vigumu kwa sababu wanakemewa mpaka na watoto wao, kwa kuwa mambo hayo yanaweza kusababisha hata njaa kwenye familia na uchumi wao kuyumba.”
Kiongozi wa mila ya Kichaga kutoka Rombo Mshili, George Kavishe, alisema dhana kwamba Wachaga hurudi nyumbani mwisho wa mwaka kufanya matambiko, sio sahihi.
Alisema wanachorudi kukifanya, ni kuienzi mila iliyo njema ya kukutana na wapendwa wao, baada ya muda mrefu wa utafutaji.
"Katika kukutana na wapendwa wao, yapo mambo mengi yanayofanyika, ikiwemo kufanya ibada za familia, kufanya usafi kwenye makaburi, kutatua migogoro ikiwa ipo, na hii ni ishara njema ya umoja na upendo.
"Usimamizi huo unaleta tija katika koo husika zipo nyakati wanapendekeza mambo ya kimaendeleo, ikiwemo kuoa, kuacha tabia zilizo mbaya miongoni mwa jamii na kuongeza ushirikiano,” alisema.
Mchili wa Wachaga wa Mwika, Laurence Mlay, zaidi alifafanua akisema: "Wako wachache kwenye jamii, ambao wanakaidi kutokana na tabia hizo kuota mizizi, ila tunahakikisha tumewachukulia hatua kwa kushirikiana na serikali.
“Wale wote wanaoshindwa kuja nyakati za sikukuu za mwisho wa mwaka, sisi tunawahesabu kama wavivu na wasiojituma hivyo serikali iwachukulie hatua."
Mangi wa Machame, Gilbert Shangali, alisema yeye kama kiongozi wa mila, hatavumilia wavivu na wanywaji wa pombe kupitiliza katika jamii ya kabila 52.
"Nitashirikiana na serikali katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, nitapinga uvivu, wizi, matumizi ya madawa ya kulevya, ukatili na utelekezaji wa watoto, wanawake na wazee,"alisema Mangi Shangali.
· Imeandikwa na Godfrey Mushi na Mary Mosha (Moshi).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED