WATU wanane wakiwamo wanafunzi watatu wamefariki dunia katika ajali zilizotokea mikoa miwili tofauti baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na mengine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, alisema watu wanne wamefariki dunia jana wilayani Babati baada ya gari la mizigo aina ya Scania kuligonga basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa na wanafunzi hao.
Alisema ajali hiyo ilitokea eneo la Gajal, wilayani Babati na kwamba chanzo chake ni Scania kuligonga basi hilo dogo lililokuwa likitokea wilayani Hanang' kwenda Arusha, likiwa na wanafunzi 33.
“Dereva wa lori alikuwa mzembe kwani alishindwa kuwa makini barabarani na kuligonga basi dogo na kusababisha vifo hivyo,” alisema Makarani
Alisema wanafunzi watatu waliokuwa kwenye basi hilo dogo walifariki dunia pamoja na dereva.
"Wanafunzi hao waliokuwa katika basi dogo walikuwa wanatoka Shule ya Sekondari Endasak wakienda likizo Arusha, baada ya shule zao kufungwa,"alisema.
Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga, alitoa pole kwa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kutokana na ajali hiyo.
"Tunamuomba Mwenyezi Mungu, awape nafuu na uponyaji wa haraka majeruhi wote wa ajali hiyo ambayo imesababisha vifo vya watu wanne,” alisema Sendiga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alisema watu wanne akiwamo dereva wa gari, wamefariki dunia katika ajali iliyotokea Kijiji cha Manchali baada ya gari hilo kugongana uso kwa uso na lori.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kutaka kulipita gari walilokuwa wakiongozana nalo na kukutana uso kwa uso na lori.
“Watu hao walikuwa wakirejea nyumbani wakitokea katika sherehe, dereva wa gari hilo, Emmanuel Kazimoto (38) pamoja na abiria wengine wawili wamekufa papo hapo, huku abiria mwingine amefariki dunia akipatiwa matibabu. Miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma,” alisema.
Kamanda Katabazi alisema Ajali zilivyoua wanane wakiwamo wanafunzi linaendelea kufuatilia madereva wazembe ambao husababisha ajali kwa kuendesha mwendokasi bila kufuata sheria za barabarani.
· Imeandikwa na Jaliwason Jasson (BABATI) na Renatha Msungu (DODOMA)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED