MBUNGE wa Bukene (CCM), Selemani Zedi, amezitaka shule nchini kutoza ada himilivu ili wanafunzi wengi wanaotoka familia zisizo na uwezo kupata fursa ya kusoma na ameipongeza shule ya St Anne Marie kwa kukubali kusomesha wanaofiwa na wazazi.
Alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya 20 ya shule ya sekondari St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.
“Dk. Jasson Rweikiza, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa shule hizi, ni maombi matatu kwako, mosi umeeleza kwenye hotuba yako kuwa ada ya hapa ni ndogo na hulipwa mara nne kwa mwaka ili kuwarahisishia wazazi ulipaji, Naomba ada ya shule zako iendelee kuwa himivu, ili watanzania wengi waweze kumudu kuwaleta watoto wao wasome kwenye shule hii ili wapate elimu bora inayotolewa hapa,” alisema.
Alisema ameambiwa kuwa shule inaishi vizuri sana na majirani na inashiriki katika kuchangia maendeleo ya jamii kama kusomesha wasiojiweza, kuchangia ujenzi /ukarabati wa barabara, shule, maji, ulinzi, usafiri, viwanja vya michezo, kumbi na huduma nyingine,”
“Naomba hili pia liendelee kwani ni jambo jema sana. Ombi la tatu, Nimekusikia pia kwenye hotuba yako kuwa shule inatoa kipaumbele kwenye ajira kwa majirani wanaozunguka shule hii, hili nalo pia ni jambo jema litadumisha uhusiano kati ya shule na majirani na kuwafanya watanzania wanoishi jirani na shule hii waendelee kuithamini na kuipenda shule hii,” alisema Mbunge huyo.
Alimpongeza Mkurugenzi wa shule, Dk Jasson Rweikiza, ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu na kamba ameisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa kuwasaidia watanzania kupata elimu bora.
“Napenda kupongeza sana uongozi wa shule kwa usimamizi mzuri wa shule. Sote ni mashahidi kwamba shule hii inafanya vizuri sana kitaaluma kwa kupata matokeo mazuri sana katika mitihani ya Taifa. Nimesikia hapa kwenye taarifa kwamba matokeo ya darasa la nne, la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kitado cha sita ni mazuri sana,” alisema.
Alisema matokeo hayo mazuri yanaonesha ni kwa jinsi gani shule hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanaohitimu hapa wanapata matokeo mazuri sana na alipongezauongozi wa shule kwa kuhakikisha huduma zote muhimu kwa wanafunzi zinapatikana na kujitosheleza.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Rweikiza alisema shule ina majii ya kutosha kwa ajili ya kupikia, kufua, kumwagilia mashamba, bustani za maua na mboga, maji safi na salama ya kunywa na kuna magari ya kusambaza maji wakati wa dharura ya maji ya DAWASA yanapokatika.
Alisema shule ina mashamba makubwa ya matunda (michungwa, nanasi, maembe n.k) na mboga za majani kwa ajili ya chakula cha wanafunzi na ina mradi wa ufugaji wa ng’ombe na kuku kwa ajili ya nyama na mayai ya wanafunzi.
Alisema wanafunzi wanaofanya vizuri wamekuwa wakipelekwa mbuga mbalimbali za wanyama kama Mikumi, Ngorongoro na Serengeti kama motisha kwa wengine kufanya vizuri na kuongeza kuwa shule ina wadhibiti ubora ambao wamekuwa chanzo cha mafanikio hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED