HUKU wakiwa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupata ushindi wa mechi mbili walizocheza, uongozi wa Simba umesema wanakiamini kikosi walichonacho kitapambana na kuwafuta 'machozi'.
Simba jana ilikuwa inacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan ili kujiimarisha kuelekea mchezo wake wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa ugenini Septemba 13, mwaka huu.
Wekundu wa Msimbazi itawafuata Al Ahly Tripoli ya Libya na baadaye itarejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Septemba 20, mwaka huu kwenye kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema timu yao imeshaanza kuwapa 'matunda' na wanaamini wachezaji wataendelea kuwapa furaha katika michezo inayokuja.
Ahmed alisema kila mchezaji anafahamu 'kiu' waliyonayo mashabiki na wanachama wa Simba hivyo jukumu lao ni kupambana na kusaka ushindi katika kila mechi watakayocheza.
"Tuna wachezaji wazuri na wakubwa, wanajua wanatakiwa kufanya nini na kwa wakati gani, pia tuna benchi la ufundi ambalo limetimia kwa ajili ya kuhakikisha malengo ya klabu yanafikiwa," alisema Ahmed.
Aliongeza wamejipanga kukutana na ushindani katika kila mechi kwa sababu wanajua timu zote zinahitaji kujiweka kwenye nafasi salama kwa kushinda michezo ya mzunguko wa kwanza.
Simba ilianza msimu huu kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United na mchezo wake wa pili ikawafunga Fountain Gate magoli 4-0.
Nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inashikiliwa na Singida Black Stars yenye pointi ikifuatiwa na Mashujaa FC ya Kigoma iliyojikusanyia pointi nne wakati Yanga inafuatia ikiwa na pointi tatu.
Fountain Gate ya Singida iliyopanda daraja msimu huu inafuatia katika msimamo huo ikiwa na pointi tatu sawa na Tabora United ya mkoani Tabora.
Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha kalenda ya kimataifa ambapo hapa nchini Taifa Stars itawakaribisha Ethiopia katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED