Wapinga kifungu sheria rushwa ya ngono

By Mary Geofrey , Nipashe Jumapili
Published at 09:18 AM Sep 01 2024
Rebeca Gyumi
Picha:Mtandao
Rebeca Gyumi

WANAMTANDAO wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania, wamepinga muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Ngono, Kifungu cha 10(b), unaotarajiwa kusomwa bungeni Jumatatu (kesho), kwa madai kinahalalisha rushwa ya ngono kwa vijana na wasichana.

Aidha, mtandao huo unasisitiza kifungu cha 25 katika sheria hiyo inajitosheleza na hakihitaji marekebisho yoyote na kiendelee kutumika, hivyo kifungu 10 (b) kiondolewe.

Mmoja wa wanamtandao hao, Rebeca Gyumi, aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu muswada huo wa sheria.

“Hoja ya msingi wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kinaeleza kuwa ili kuwe na rushwa, lazima kuwe na mtoaji na mpokeaji. Kwa nini rushwa ya ngono inamwangalia mpokeaji tu?” alihoji. 

Gyumi aliwaomba wabunge kutopitisha muswada huo, kwa ajili ya maslahi mapana ya waathirika wa rushwa wa ngono nchini.

“Sisi wanamtandao tunataka wanaoendelea kupigia debe mabadiliko haya, wasipotoshe umma kwa kuchanganya dhana ya rushwa, mshawishi, anayeshawishi na anayeshawishika," alisema Gyumi.

Mwanamtandao na Mwanaharakati, Dk. Ananelia Nkya, alisema, "Wabunge wakipitisha kifungu hicho, wataliangamiza taifa kwa kuhalalisha matukio ya rushwa ya ngono.” 

Alisema muswada huo pia ukipita si tu utadhalilisha utu wa wanaofanyiwa ukatili wa rushwa ya ngono, bali pia unamdhalilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Wanamtandao hao na washiriki wote wanaopigania haki za binadamu na makundi ya pembezoni, kutoka takribani asasi 200 kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa.

Mtandao huo pia, ulihusika na uchambuzi yakinifu wa mapendekezo ya awali ya marekebisho ya sheria hiyo na kutoa tamko lao kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).