WAKAZI wa kijiji cha Ngokolo, Kata ya Bukomela Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, walioishi miaka yote bila kuwa na huduma ya mawasiliano, wameeleza hali hiyo ilivyowatesa hadi kuwalazimu kuitafuta kwa kupanda juu ya miti na milimani.
Walieleza hayo juzi kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa mnara wa mawasiliano katika maeneo hayo uliozinduliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, huku wakisema hatua hiyo imewasaidia kuondokana na adha hiyo.
Mmoja wa wananchi hao, Joseph Mabala, alisema kijijini hapo hapakuwa na mawasiliano kabisa na kwamba walikuwa wakipanda juu ya miti na milimani ndipo wapate kuwasiliana.
"Tunashukuru kupata mnara wa mawasiliano hapa kijijini, tatizo la kupanda juu ya miti na milimani halipo tena, sasa hivi tunawasiliana tu sehemu yoyote," alisema Mabala.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, alisema hali ya mawasiliano jimboni humo si nzuri kutokana na ukosefu wa minara na kuwa waliomba kuwekewa minara saba lakini iliyokamilika ni minne na kusalia mitatu na kumwomba waziri kukamilishwa kwa iliyosalia.
Waziri Nnauye alisema kwa sasa wanatekeleza mradi wa nchi nzima ujulikanao kama Tanzania ya kidijitali kwa kujenga minara 758 katika mikoa 26 Tanzania Bara, ili kurahisiha hali ya upatikanaji wa mawasiliano hasa maeneo ya vijijini ambayo hayakuwa na huduma hiyo matarajio yakiwa kuwafikia Watanzania milioni 8.5.
Alisema katika mkoa wa Shinyanga, inajengwa minara 30 na katika jimbo hilo itajengwa minara saba na kwamba minara minne tayari imekamilika na kusalia mitatu ambayo nayo itakamilishwa kujengwa hivi karibuni na kuwashwa.
Aidha, aliwatahadharisha wananchi wa kijiji cha Ngokolo na maeneo mengine ambayo minara hiyo tayari imeshawashwa na kupata mawasiliano, kwamba wachukue tahadhari kuepukana na matapeli wa mitandaoni wakiwamo wa tuma kwa namba hii ili kutotapeliwa pesa zao wakiwamo na wastaafu.
Pia aliwasihi vijana wasitumie mitandao ya kijamii kwa matumizi yasiyo sahihi, kwa kuchafuana na hata kutukana viongozi, ili wasije ingia kwenye mikono ya sheria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED