Stand United yapania kurejea Ligi Kuu Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 01:56 PM Dec 22 2024
Stand United
Picha: Mtandao
Stand United

TIMU ya Stand United imeonesha kudhamiria kurejea Ligi Kuu, baada ya kuitwanga Cosmopolitan mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi ya Championship, uliochezwa juzi, Ijumaa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo kupanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo, ikifikisha pointi 26, ikiwa ni moja nyuma ya Geita Gold inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 27 na tatu nyuma ya Mtibwa Sugar ambao ni vinara wa ligi hiyo ikiwa na pointi 29.

Hata hivyo, Standa United iliyoshuka daraja msimu wa 2020/21, imecheza michezo 13, ambao ni mmoja zaidi ya timu hizo mbili zilizo juu yake, zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita.

Mabao ya washindi yalifungwa na Emmanuel Manyanda, dakika ya 28 na 83, la kwanza likiwekwa wavuni dakika ya 24 na Lucas Sendama.

Mechi nyingine iliyochezwa juzi, Uwanja wa Kituo cha TFF, Mnyanjani jijini Tanga, wenyeji Africa Sports walijikuta wakipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya Kwanza.

Ushindi wa Mbeya Kwanza unaifanya timu hiyo kufikisha pointi 24 na kupanda hadi nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.

Ikumbukwe kuwa timu mbili zitakazoshuka nafasi mbili za juu mwishoni mwa msimu zitapanda moja kwa moja Ligi Kuu, huku mshindi wa tatu na wa nne wakicheza mechi za mchujo na mshindi ataisubiri timu ya Ligi Kuu kucheza nayo pia mechi ya 'play off.'

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mbuni FC iliitandika Kiluvya mabao 3-1, yakitiwa kwenye kamba na Michael Mwingwa aliyefunga mawili na Advent Pius.

Pointi tatu ilizopata Mbuni zinaifanya kufikisha alama 19, ikiwa kwenye nafasi ya nane ya msimamo wa ligi hiyo, huku Kiluvya FC ikikamata mkia, ikiwa na pointi nne tu katika michezo 13 iliyocheza mpaka sasa.