UWT waonya watendaji kuhusu rushwa

By Gideon Mwakanosya , Nipashe Jumapili
Published at 01:29 PM Dec 22 2024
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda

MWENYEKITI wa Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amekemea tabia za baadhi ya makatibu wa mikoa na wilaya wa jumuiya hiyo kutoa zawadi za Sh.10,000, kanga na vitenge kwa wajumbe wa umoja huo kwa malengo yao binafsi.

Amesema tabia hiyo ni kinyume cha taratibu za chama na hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo.

Chatanda aliyasema  hayo jana kwenye hafla  ya  ugawaji wa misaada  iliyoandaliwa na Mbunge Viti  Maalum Mkoa wa Ruvuma, Jacklin Msongozi, katika ukumbi wa mikutano wa Familia Takatifu, Bombambili, Manispaa ya Songea.

Misaada iliyotolewa ni mashine 20 za kukamulia alizeti, vyerahani 700, majiko banifu 300 ya gesi, mifuko ya simenti 100, mikeka ya nyumba za ibada misikiti minne   na ng'ombe wawili wa maziwa kwa familia mbili zenye kipato duni.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali wanaotengeneza mianya ya rushwa kwa wajumbe kwa kuwapa pesa na vitenge.

Chatanda alisema UWT  kwa kushirikiana na kamati za maadili, haitawafumbia macho watu hao na kusisitiza kuwa  hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema viongozi wa UWT wanapaswa kutoa huduma kwa jamii kwa kujali na si kwa manufaa  binafsi  na kuhimiza uwazi na maadili bora katika uongozi  na si vinginevyo.

"Twendeni tukawatumikie wanawake wana changamoto chungu nzima. Twendeni  tukawatembelee wanawake tuzungumze nao, tutafute fursa kama hizi ambazo amefanya Mbunge Msongozi tuwapelekee. Ukimwezesha  mwanamke umeliwezesha taifa zima.

"Lakini na wao nawaambia kwamba marufuku kuwafuata wale wanaowapigia kura na hii nawaambia ukweli hatuwatendei haki wanawake wale ambao waliwachagua kwa kuwapa Sh.10,000, "alisema Chatanda.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawategemea sana wanawake walioko kwenye vijiji kwa kuwa ndio  wanaokiwezesha kushinda, hivyo ni lazima wawatembelee, wazungumze  nao ili wajue changamoto zao  na kuzifanyia utatuzi kama alivyofanya Msongozi.

Chatanda alimpongeza Msongozi kwa kuwa miongoni mwa wabunge wachache wanawake ambao wanafanya vizuri kwa kuwainua wanawake na makundi mengine.

Msongozi alisema wamegawa vifaa hivyo ili kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana wa mkoa huo kujikwamua kiuchumi ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.

Tukio hilo liliambatana na utoaji wa  taarifa ya utekelezaji  wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025 katika sekta za kilimo, ufugaji, viwanda, nishati, elimu na lishe.

Alisema uhitaji wa mafuta nchini ni mkubwa wakati uzalishaji ni mdogo, akibainisha kuwa uzalishaji huo kwa sasa nchini  ni tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji ya mafuta ya kula ambayo ni tani 650,000 kwa mwaka

Ofisa Biashara wa Mkoa wa Ruvuma, Joseph Martin, alisema  kwa kushirikiana na mbunge huyo, ofisi yake  itatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanavikundi wote juu ya utunzaji wa kumbukumbu za hesabu, ufungashaji, umuhimu wa usajili wa biashara, taratibu za uendeshaji wa biashara kwa kufuata sheria za kibiashara, kujitangaza kibiashara na mambo mengine.