Wazee wataka bima maalum ya afya

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 02:27 PM Dec 22 2024
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, akitoa maoni wakati wa mkutano wa wazee katika kuhakiki rasimu ya dira ya taifa ya maendeleo 2050.
Picha zote: Maulid Mmbaga.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, akitoa maoni wakati wa mkutano wa wazee katika kuhakiki rasimu ya dira ya taifa ya maendeleo 2050.

KUELEKEA mwaka 2050, wazee nchini wameomba kuwa katika Bima ya Afya kwa Wote, kundi la hilo litambuliwe kwa kupatiwa bima maalumu itakayowawezesha kupata matibabu bila malipo ili kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, leo, wakati akizungumza katika Mkutano na baraza hilo wa kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema kuwa wazee wanaomba utoaji wa huduma za matunzo na kisaikolojia hasa wale walio katika maeneo ya vijiji kujumuishwa katika Dira 2050. Halikadhalika wameomba wazee washirikishwe katika ngazi za maamuzi ya vijiji, mtaa mpaka taifa.

"Pia tunashauri haki ya wazee ya  kuishi maisha bora yenye utu kwa kuheshimiwa na haki ya usawa mbele ya sheria pasipo ubaguzi dhidi ya yetu zizingatiwa katika Dira 2050," amesema.

Mkutano na baraza hilo wa kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
"Pia tunapendekeza masuala ya wazee hasa ustawi, kuzingatiwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050  kwa kuimarisha, kusimamia na kufuatilia huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma, vya serikali na binfasi ili kuendana na mahitaji yao," amesema.

Ameongeza kuwa wazee wanahitaji  mabaraza maalumu ya kujengewa uwezo ili kutekeleza majukumu kikamilifu ikiwamo kutoa ushauri kwa jamii, kulinda mila na desturi.

Pia wametaka kuwepo kwa sheria ya wazee itakayowawezesha upatikanaji na utekelezaji wa huduma kwa kundi hilo kama stahiki, kwa mujibu wa sera ya wazee na nyingine.