DC Magoti: Ukitoa taarifa ya mtoto anayechezwa unyago nakupa 50,000

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 09:38 PM Jul 14 2024
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti.
Picha: Julieth Mkireri
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti.

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema mwananchi wa wilaya hiyo atakayetoa taarifa ya mtoto anayechezwa unyago atatoa zawadi ya fedha taslim shilingi 50,000.

Amesema atakayehusika kucheza mtoto wake sheria itachukua mkondo wake kwani hali hiyo imekuwa ikichangia kuharibu maisha ya baadae ya mtoto.

"Mnapocheza ngoma watoto wengine wanacheza kuliko wanawake na kusababisha kubakwa hii ni hatari kwa watoto," amesema

Akizungumza katika mkutano na wanannchi uliofanyika leo Julai 14 katika Kijiji cha Homboza Kata ya Msimbu wilayani humo Magoti amesema hatakalia kimya suala hilo ambalo linachangia vitendo vya kikatili kwa watoto.

1

Amesema Kisarawe ni kati wilaya ambazo zina shule nyingi na serikali imekuwa ikipeleka fedha huko kuwezesha huduma ya elimu hivyo wananchi wanatakiwa kutilia mkazo elimu badala ya Ngoma.

"Ukipata taarifa zilizothibitika kuna mtu anacheza unyago mtoto chukua pikipiki njoo ofisini nitakupa sh. 50,000 na nikifika eneo la tukio nitaondoka na baba wa mtoto, aliyeleta miziki, mshauri wa unyago na wengine waliohusika sheria itachukua mkondo wake," amesisitiza.

Amesema utaratibu huo utaendelea Ili kuwezesha Wilaya hiyo kuwa na mabadiliko ya kielimu na kukomesha vitendo vya ubakaji ambavyo vinachangiwa na ngoma hizo.