Ngogongoro Heroes, Rwanda hatumwi mtoto CECAFA U-20

By Somoe Ng'itu , Nipashe Jumapili
Published at 08:15 AM Oct 13 2024
Baadhi ya Wachezaji wa Ngogongoro Heroes.
Picha: Mtandao
Baadhi ya Wachezaji wa Ngogongoro Heroes.

TIMU ya Taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), inatarajia kuikaribisha Rwanda katika mechi ya Kundi A itakayochezwa leo, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Ngorongoro Heroes yenye pointi sita sawa na Sudan ndio vinara wa Kundi A wakati Rwanda iko katika nafasi ya nne, ikiwa na pointi mbili.

Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Boniface Mkwasa, amesema timu yake iko tayari kwa ajili ya mchezo huo na wataongeza umakini, kwa sababu Rwanda watashuka dimbani wakiwa hawana presha yoyote.

Mkwasa alisema anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu, lakini kikosi chake kitaingia tofauti kulingana na mpinzani wanayekutana naye.

"Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu wa hatua ya makundi, tunajua hautakuwa mchezo rahisi, lakini tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi na kuongoza kundi letu," Mkwasa alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Rwanda U-20, Eric Nshimiyimana, amesema mechi hiyo dhidi ya wenyeji itakuwa ngumu, lakini amewaandaa wachezaji wake kucheza soka la ushindani.

"Haitakuwa mechi rahisi, tunajua Tanzania wanataka kujihakikisha tiketi ya kusonga mbele, lakini sisi pia hatutaki kupoteza, nimewakumbusha wachezaji kucheza kwa kuwaheshimu wapinzani," alisema kocha huyo na kiungo wa zamani wa APR na Amavubi.

Aliongeza amefanyia kazi mapungufu na anaamini wataingia katika mechi hiyo  wakiwa imara.

Tayari Uganda na Burundi zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya fainali ya michuano hiyo, itakayofanyika Oktoba 18, mwaka huu na fainali ikichezwa siku mbili baadaye.