MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, amesimikwa rasmi kuwa Mtemi wa Buduhe na kupewa jina la Nyangindu wa tatu.
Hafla hiyo ya kusimikwa kuwa Mtemi wa Buduhe imefanyika jana katika Himaya ya Buduhe Kata ya Kishapu, na kuongozwa na Utemi wa Busiya.
Francis Izengo Nyangindu akisoma historia fupi ya Utemi wa Buduhe, amesema ulianza mwaka 1714-1962 ambapo kulikuwa na ugomvi wa watoto wawili, na kwamba mtoto mdogo alichaguliwa atawale eneo la Utemi wa Nyashimba, na mkubwa akataka kuanzisha ugomvi, lakini Wagonhg'ogonhg'o walimshauri ahame na kwenda sehemu ya kusini eneo ambalo halina watu.
Amesema mtoto huyo mkubwa aliondoka na watu ambao walikuwa wakimuunga mkono, na ndiyo akawa Mtemi wa kwanza wa Kishapu jina lake Butondo Nkulu Ngw'ana Gimbi, ambaye alianza kutengeneza Himaya katika eneo lililokuwa likitawaliwa na watu wa kuhamahama (Basunga), ndipo wakamuuliza "U-Buduhe" yani ukubwa wenu mnatoka wapi, na kisha likazaliwa neno Buduhe, na jina halisi lilikuwa Kumbayu Ng'wabusele.
Amesema baada ya mwaka 1720 katika eneo hilo wakatawala Watemi wengine, ambao wanatokana na Himaya ya Chifu Butondo upande wa wanawake (Bakumigongo), na kwamba eneo hilo kulikuwa na Wanyama wakali kama vile Simba, na Wasagi wa unga wa Mtemi walikuwa wana saga kwa mawe, na Simba walipokuwa wakisikia Muungurumo wa wasagi walikuwa wakiwavamia.
Amesema kutokana na tatizo hilo, ndipo ikatoka amri ya Mtemi kwamba muwe mnasaga kuanzia asubuhi hadi jioni usiku hapana(NG'HYUYUSHA PUU)ndipo likazaliwa neno Baji Shapuu.
Anasema baada ya hapo watu wa maeneo mbalimbali,wakawa wanasema "duje kubajishapuu" na eneo hilo likajulikana kama Jishapu na siyo Kishapu.
"Eneo hili la Jishapu Watemi waliotawala hadi sasa ni 15 , kulingana na Uchifu wa miaka iliyofuata Watemi wengine kama Nyangindu na Luhende walitoka Himaya ya Usia, kama Izengo Ng'wabajimisha Manoni, ambaye alimzaa Sondo na Sondo alimzaa Nyangindu wa pili (11) na Nyangindu akamzaa Luhende ndiyo Mtemi wa 14, na Buduhe imezaliwa na Usia kwa utawala,
Aidha, amewataja Watemi wa Buduhe ambao wametawala tangu mwaka 1714 hadi 1962, kuwa ni Butondo Mkuu Ng'wanagimbi aliyetawala kuanzia mwaka 1714 -1720, Kimali (1) Ng'wana Nyanzobe 1720-1742, Mafunda Ng'wana Yunga 1743-1753, Songoyi Ng'wana holo 1753-1755,Nyangindu(1) Ng'wana sele 1756-1758, Mulawa Ng'wanaholo 1759-1799, Jibalo Ng'wanaholo ambaye alitawala nusu mwaka 1799.
Wengine ni Ng'wika Bugeleja Nyanzobe 1800-1830, Jitanita Ng'wanadilu, Butondo Ng'wanamondea (11)1835-1840, Kimali (11)Ng'wana Mbuke 1841-1891,Mafunda (11)Ng'wana Ng'walu, 1892-1903,Nyangindu (11)Ng'wanaduke 1904-1911, Luhende Hollo Nyangindu 1911-1930, Nshoka Luhende 1931-1962 na Mtemi wa 16 ni Nyangindu Ng'wana Butondo (111) 2024 na kuendelea..
Naye Mtemi Nyangindu (Butondo) akizungumza mara baada ya kusimikwa kuwa Mtemi wa Buduhe, ameomba ushirikiano, huku akihidi kushirikiana na Watemi wengine kutoka maeneo mbalimbali.
Aidha,amewawasihi wananchi wa Kishapu, kwamba msimu wa kilimo 2024/2025 kutakuwa na mvua chache kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa, ambapo wanapaswa kulima mazao ambayo yanastahimili ukame.
Ametaja mazao hayo kuwa ni Mtama,Alzeti,Viazi Vitamu,Dengu,Choroko, na kwamba wale ambao wapo mabondeni ndiyo wanaweza kulima Mahindi.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amepongeza Tamaduni hizo za Watemi, na kwamba serikali itaendelea kushirikiana nao Watemi katika shughuli mbalimbali pamoja na kudumisha Amani ya nchi.
Amewasihi pia wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye datfari la wakazi,ambalo limeanza jana Oktoba 11 litakalo kwenda hadi tarehe 20, ili Novemba 27 wapate fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuchagua viongozi wazuri watakaowaletea maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED