RIPOTI MAALUMUlaji chipsi ulivyobadili utaratibu wa mlo kamili

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:31 AM Oct 13 2024
Chipsi kuku
Picha: Mtandao
Chipsi kuku

CHIPSI kuku, chipsi yai au chipsi mishkaki kimekuwa chakula maarufu miongoni mwa watu wa marika yote. Si kinababa, kinamama, vijana wa kike na wa kiume.

Ulaji wa aina hiyo ya chakula, umetajwa kubadili matumizi ya chakula bora na mlo kamili, kwa sehemu kubwa ya familia nchini pamoja na mtu mmoja mmoja.

Awali, ulaji wa chakula hicho ulionekana kukithiri zaidi Dar es Salaam, ukaenea hadi miji mikubwa na midogo na sasa hadi vijijini umejipatia umaarufu.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe Jumapili, umebaini sehemu ya kubwa ya familia za mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinatumia chakula hicho kama sehemu ya milo mitatu na kusahau utaratibu wa mlo uliozoeleka kama vile ugali na wali, kwa kula pamoja na nyama, samaki, mboga na maharage.

Mkoani Kagera, baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe, akiwamo Rozalia Mjumba, mfanyabiashara wa Soko Kuu la Bukoba, anasema kubanwa na majukumu ndiyo sababu ya kugeukia chakula hicho.

Anasema kutokana na kubanana na shughuli mbalimbali katika kazi zake, hulazimika kuagiza chipsi na wakati mwingine kuondoka na chakula hicho kwenda nacho nyumbani, kwa ajili ya familia yake. Anasema muda anaotoka kazini, anakuwa hana uwezo tena wa kuandaa chakula kingine.

"Chakula changu ninachokipenda zaidi ni chipsi iliyochanganywa na yai. Inakuwa  na gharama kidogo Sh. 2,500. Nikinunua na pepsi ni 3,000 jumla ambayo naiona hainigharimu sana. Lakini  nikiwa nyumbani, wakati mwingine naweza kula wali au ugali na mboga za majani, nyama au samaki. Ninapopata  muda wa kuandaa chakula hicho," alisema.

Mjumba ambaye ni mkazi wa Kata ya Miembeni, Manispa ya Bukoba, anasema wakati mwingine hata akiwa nyumbani, anaagiza bodaboda kumpelekea chipsi, kwa ajili yake na familia ya watoto watatu, kwa kwa kuwa ndicho chakula wanachokipenda.

“Nikila chipsi nalala na naamka vizuri na ni muda mrefu utaratibu wangu ni huo.  Sijawahi  kupatwa na magonjwa ya aina yoyote tofauti na kuona ongezeko la mwili, ambao hauna madhara kwangu,” anasema.

Mkazi wa Nyasaka, mkoani Mwanza, Rebeca Nkaila, anasema mazingira ya upatikanaji wa chakula hicho mahali pa kazi pamoja na gharama, ndiyo sababu inayomfanya yeye pamoja na wengine kukimbilia chipsi.

Naye Mkazi wa Majengo, wilayani Magu mkoani Mwanza, Khadija Idd, anasema chakula chake pendwa ni chipsi kwa sababu ni  chakula rahisi cha haraka ambacho kinaweza kuliwa muda wowote bila kikwazo. Pia anasema maandalizi yake ya muda mfupi ni tofauti na kuanza kuandaa ugali au wali na mboga.

Mkazi wa Kijiji cha Ihayabuyaga, Magu mkoani Mwanza, Omary Kassim. anasema anatambua chakula hicho kuwa kina athari za kiafya ikiwamo uzito kupita kiasi, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, kutokana na mafuta mengi na chumvi zinazotumiwa kwenye maandalizi. Pamoja na kutambua athari za chakula hicho, anasema  yote hayo wanamwachia Mungu.

Ni wazi kwamba ulaji wa chakula cha aina hiyo, una madhara kwa afya ya mtumiaji na wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza watu kuchukua tahadhari.

Aidha, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava, hivi karibuni, aliwashirikisha ujumbe wa Mwenge akisema wananchi wazingatie utumiaji wa vyakula vyenye lishe bila kusahau matunda na mboga, ili kuboresha afya zao na kuacha kutumia vyakula ambavyo vinajaza tumbo.

WAUZA CHIPSI WALONGA

Wafanyabiashara na watengenezaji wa chipsi, kutokana na chakula hicho kuchangamkiwa, wanasema wana uhakika wa kuuza wastani wa gunia moja na mafuta wastani wa lita 16 hadi 18 kwa siku, biashara ikiwa ya kawaida.

Mfanyabiashara katika eneo la Hamgembe mkoani Kagera, Godwin Elias, anasema kutokana na biashara hiyo kuonekana kupendwa, vijana wengi wameamua kuwekeza, hivyo kufanya idadi ya wauzaji kuwa kubwa na kuanza kugawana wateja.

Mfanyabiashara mwingine kutoka Malimbe jijini Mwanza, Emmanuel Kapesa, anasema wateja wengi wa chakula hicho ni wanawake kulinganisha na wanaume.

Anasema upatikanaji wa malighafi za chakula umerahisisha maandalizi ya chakula hicho na kukifanya kuwa chaguo la watu wengi, hasa wafanyabiashara ambao wana majukumu mengi na kukosa muda wa kuandaa chakula chenyewe.

WATAALAM WAONYA

Ofisa lishe Mkoa wa Shinyanga, Yussuf Hamis, anasema kula chipsi si tatizo, bali tatizo ni matumizi ya muda mrefu hali inayozidisha kiwango cha vitu vinavyohitajika, ikiwa ni pamoja na kutokuzingatia mlo kamili.

“Si rahisi kubaini kama kuna madhara kwenye ulaji wa kupindukia wa vyakula vyenye mafuta mengi kupita kiasi kama chipsi. Lakini  wanachotakiwa kutambua ni kuwa uandaaji wake hutumia mafuta mengi ambayo yakiingia mwilini pamoja na kiwango kikubwa cha wanga, husababisha magonjwa yasioambukiza yakiwamo kisukari,  maradhi ya moyo, na shinikizo la damu,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, Dk. Bahati Msaki, magonjwa yasiyoambukiza yatokanayo na ulaji usiofaa, yamezidi kuongezeka kwa kasi, hivyo kuwa miongoni mwa magonjwa 10 tishio.

Dk. Msaki anasema magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, unaoshika nafasi ya kwanza kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kwa watu wazima. Anasema katika hospitali hiyo, ugonjwa huo una wagonjwa 5,589 huku kisukari kikishika nafasi ya tano, kwa kuwa na wagonjwa 2,778.

Ofisa Lishe Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Abel Gyuga, anasema kumekuwa na  ongezeko la wagonjwa wa magojwa yasiyoambukiza, kama shinikizo la juu la damu (BP), kisukari, vidonda vya tumbo, saratani na figo, kutokana na ulaji usiofaa na kuacha kula milo kamili kama inavyotakiwa.

Gyuga anasema takwimu za mwaka 2022 zinaonesha wagonjwa 2,372 wa nje waliokuwa wanaendelea kuchukua dawa kati ya hao, wagonjwa wa BP walikuwa wanaume 863 na wanawake 1,509; kisukari 671 wakiwamo wanaume 301 na wanawake 370.

Pia anasema waliolazwa katika hospitali ya wilaya kwa mwaka huo, 219 walikuwa na shinikizo la damu wanaume wakiwa 63 na wanawake 116, kisukari 26 kwa wanaume tisa na wanawake 17.

“Ukiangalia takwimu  hizi wanawake wamekuwa waathirika wa maradhi haya na hii inatokana na mtindo wa maisha. Kwa  sasa wakitumia kwa wingi vyakula vyenye mafuta ikiwamo chipsi na mambo mengine kama pombe kupita kiasi, sigara, kutofanya mazoezi na kutokula mlo kamili unaozingatia makundi matano ya lishe, yakiwamo mboga na matunda,” anasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Kisukari Tanzania (TDA), Prof. Andrew Swai, anasema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi  na kuwaathiri watu wengi, wakiwamo watoto. Anabainisha kwamba vifo milioni 42 sawa na asilimia 71 duniani kote vilivyohusisha watu wa umri wa miaka 30-70 vilisababishwa na maradhi yasiyoambukiza.

“Mtu anaweza kuwa na magonjwa yasiyoambukiza kwa miaka kadhaa, bila dalili huku mwili ukiendelea kuathirika. Mfano  shikizo la juu la damu, pia kisukari unaweza usiwe na dalili hadi macho, figo, moyo au mishipa ya damu au fahamu inapokuwa imeharibika vibaya, hivyo tunahitaji kubadili ulaji wetu,” anasema.

Prof. Swai anasema kila mtu ahakikishe uzito unakuwa katika kiwango kinachofaa, kupunguza unywaji wa pombe na matumizi ya tumbaku.

Anasema matibabu ya magonjwa ya figo, moyo na kisukari ni ya gharama kubwa na yanatumia asilimia nne ya pato la taifa pia wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambao wanasumbuliwa na maradhi hayo, wanatumia asilimia 20 ya mfuko. 

·      Imeandaliwa na Restuta Damian (KAGERA), Remmy Moka (MWANZA), Neema Emmanuel (MAGU), Vitus Audax (MWANZA), Alex Sayi (MASWA).