Ndejembi asifu kamati kujenga vyumba vya madarasa na kubakiza chenji

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 04:46 PM Oct 06 2024
Ndejembi asifu kamati kujenga vyumba vya madarasa na kubakiza chenji
Picha: Shaban Njia
Ndejembi asifu kamati kujenga vyumba vya madarasa na kubakiza chenji

Kamati ya Shule ya Sekondari Ntobo, Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga, imefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa vyumba saba vya madarasa kwa gharama ya Shilingi milioni 170.8 badala ya Shilingi milioni 182 zilizotengwa, na kubakiza chenji ya Shilingi milioni 11.1. Hali hii imemshangaza Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, kutokana na ufanisi huo adimu katika utekelezaji wa miradi ya umma.

Waziri Ndejembi alionesha mshangao wake baada ya kusikiliza taarifa iliyotolewa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ntobo, Hussein Mbwambo, kuhusu ujenzi wa madarasa hayo saba pamoja na matundu nane ya vyoo vya wanafunzi, ofisi moja ya walimu, na ufanisi uliopelekea kubakiza chenji kwa kila mradi. Kamati ya shule hiyo imeomba idhini ya kutumia fedha zilizobaki kukarabati jengo la utawala. 

Waziri Ndejembi asifu uadilifu wa Kamati ya Ujenzi

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo, Waziri Ndejembi alisifu juhudi na uwajibikaji wa kamati ya ujenzi kwa kutumia fedha kwa ufanisi. "Kwa kawaida, mara nyingi tunapokea taarifa za miradi ya maendeleo ambapo fedha huisha kabla ya mradi kukamilika au mradi unakamilika chini ya viwango," alisema Ndejembi. "Lakini hapa Ntobo, miradi imekamilika kwa kiwango cha juu na chenji imebaki. Niwaombe muendelee kuwa wazalendo na kutunza miradi hii ili iweze kunufaisha wanafunzi kwa muda mrefu."

Ndejembi aliongeza kuwa ujenzi wa madarasa hayo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, na hivyo kuwapa mazingira bora ya kujifunza na kufikia ndoto zao. Aliahidi kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ili fedha zilizobaki zitumike kukarabati jengo la utawala la shule hiyo.

1

Mwalimu Mkuu afafanua matumizi ya fedha

Mwalimu Mkuu Hussein Mbwambo alitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa shule ilipokea Shilingi milioni 182 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba, lakini ilitumia Shilingi milioni 170.8, na kubakiza Shilingi milioni 11.1. Pia, kwenye mradi wa ujenzi wa matundu nane ya vyoo, walitumia Shilingi milioni 13.5 kati ya Shilingi milioni 14.4 walizopokea, na kubakiza Shilingi 940,450.

Mbwambo alieleza kuwa, kwa ujumla, miradi yote ya ujenzi imetekelezwa kwa mafanikio na imekamilika, huku ikianza kutumika na wanafunzi. Alisisitiza kuwa madarasa hayo mapya yameboresha mazingira ya kujifunzia, na sasa wanafunzi wana viti na meza 315 zinazowawezesha kusoma katika mazingira bora zaidi.

RC Macha, Mbunge waunga mkono juhudi za uboreshaji

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alipongeza ujenzi huo wa kisasa, akibainisha kuwa madarasa hayo yana miundombinu bora ikiwa ni pamoja na vifaa vya watu wenye ulemavu, vigae, na feni, na kuongeza kuwa aina hii ya madarasa imekuwa ikionekana katika shule za binafsi, lakini sasa inapatikana hata kwenye shule za serikali.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Iddi Kassimu, alisema kuwa jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu zinaendelea katika jimbo hilo. Alibainisha kuwa Sekondari ya Bulyanhulu inajenga vyumba 11 vya madarasa, huku shule nyingine kama Kabale, Ikinda, na Busindi nazo zikifaidika na uboreshaji huo. Kassimu alisisitiza kuwa kufikia mwaka ujao, hakutakuwa na uhaba wa madarasa wala matundu ya vyoo katika shule nyingi za jimbo hilo.

Mbunge huyo pia alieleza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 12 zinatumiwa kujenga chuo cha ufundi na chuo cha uuguzi, ambavyo vitasaidia kuwapa fursa vijana ambao hawataweza kuendelea na kidato cha tano kupata mafunzo ya ufundi stadi na uuguzi, na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

2