RAIS Samia Suluhu Hassan amepongeza walimu 5000 wa shule za msingi na sekondari Jijini Arusha kupatiwa mitungi ya gesi ya oryx na majiko yake kwa lengo la kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia .
Akizungumza kwa njia ya simu wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi na majiko hayo yaliyotolewa na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa uratibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Rais Samia ameonyesha kuridhishwa na hatua hiyo huku akiahidi kuongeza majiko zaidi kwa walimu hao kwa siku za baadae.
“Nimepiga simu niwapongeze walimu kwa mkutano mzuri, mbunge ameniambia leo mnamkutano wa nishati safi ya kupikia kwa hiyo niwapongeze kwa kuibeba hiyo ajenda. Niwaahidi mchango wangu katika hilo ndugu walimu katika majiko yatakayotoka mimi nitakuja kujazia baadae,” amesema Rais Samia.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga aliyekuwa mgeni katika maadhimisho ya walimu jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda amesema wanamshukuru Rais Samia kwa jitihada anazofanya za kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Katika siku hii ya leo ya kuadhimisha siku ya walimu kauli mbiu yetu inahusu masuala ya nishati safi ya kupikia na kama mnavyofahamu Rais Samia Mei mwaka huu alizindua kampeni hii ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia na malengo yetu kama serikali ni kuhakikisha itakapofika mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wamefikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia," amesema.
Aliongeza kwa kumshukuru pia Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo pamoja na Oryx kwa kutoa mitungi ya gesi kwa walimu ili watumie nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa kampeni ya Rais aliyotangaza Mei 8, mwaka huu ni kwamba kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia.
“Wizara ya Elimu tumelibeba jambo hili na tumeanza na taasisi zote za elimu ambazo zinahudumia watu zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia. Walimu 5000 wa Arusha ambao wamepatiwa majiko ya gesi wanaandaliwa utaratibu wa kupatiwa elimu ya matumizi sahihi ya nishati ili waweze kuishusha kwa wananchi na wote tutumie nishati safi.
“Rais Samia alishatoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa wabunge wote na katika Bunge lililopita kila mbunge alipewa majiko 200 kwa ajili ya kwenda kugawa katika majimbo yao na lengo kubwa ilikuwa kuhamasisha wanasiasa lakini kama mnavyofahamu jambo lolote haliwezi kwenda kama hakutakuwa na utashi wa kisiasa, hivyo Rais anatuongoza katika kampeni hii,” amesema Kipanga.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema kwa kushirikiana na mbunge huyo wameweza kuratibu walimu 5000 kupatiwa majiko hayo yenye thamani ya Sh. Milioni 417.5 lakini dhamira yao ni kuona makundi mbalimbali yakiwemo ya walimu wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Naomba niwagusie waalimu na maprofesa sio tu kwa sababu tunawasherehekea leo siku ya walimu bali naamini ninyi nyote ni kiungo muhimu kwa jamii na taifa letu. Hivyo natoa ombi maalum kwa walimu kuwa mabalozi wa Nishati Safi ya kupikia," amesema.
Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema wanatambua mchango wa walimu wote na katika kusherehekea siku ya walimu wameona kuna kila sababu ya kuwapa zawadi ya jiko la gesi kwa kila mwalimu na wao wakawe mabalozi wa nishati safi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED