Majaliwa aipongeza DAWASA kuchagiza matumizi ya Nishati safi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:05 PM Oct 06 2024
 Majaliwa aipongeza DAWASA kuchagiza matumizi ya Nishati safi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Majaliwa aipongeza DAWASA kuchagiza matumizi ya Nishati safi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaaam (DAWASA) kwa kuchagiza agenda ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia kupitia utekelezaji wa Mradi wa uchakataji topetaka (Fecal Sludge Treatment Plant) katika Kata ya Somangila Wilayani Kigamboni.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaleta manufaa ya matumizi ya nishati ya kupikia kwa Wananchi na Wakazi wa Wilaya Kigamboni na maeneo jirani.

"Niwatake DAWASA mshirikiane na Sekta binafsi katika kutoa huduma hii ikiwezekana kila Wilaya iwe na mradi kama huu wa mfanano ili Wananchi wetu wapate Nishati safi ya kupikia kama ambavyo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Samia Suluhu Hassan inasisitiza" amesema Majaliwa.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 88 na ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha nishati safi ya gasi itakayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia majumbani.

DAWASA inatekeleza miradi ya ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchata topetaka katika maeneo ya Wilaya za Kigamboni (Gezaulole, vijibweni na Golani) na katika Wilaya ya Ubungo (Kisopwa na Vikunai) na Wilaya ya Temeke (Vikunai) yenye thamani ya Shilingi Bilioni 16.