Mkurugenzi Mstaafu KCMC afariki dunia

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:21 PM Oct 06 2024
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Prof. John Shao (80)
Picha:Maktaba
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Prof. John Shao (80)

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Prof. John Shao (80) amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini humo.

Taarifa ya tanzia iliyotolewa kwa umma na Katibu Mtendaji wa Shirika la Msamaria Mwema (GSF) na Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga, Prof. Shao alikutwa na mauti leo Oktoba 6,2024. 

Alisema Prof Shao aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa GSF, Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira Mstaafu.

 “Prof. Masenga anatoa pole kwa familia, wafanyakazi wa GSF/KCMC, wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira na vyuo vyake vishiriki pamoja na wote walioguswa na msiba huu.Mwenyezi Mungu awajaze faraja katika kipindi hiki cha huzuni ili waweze kupokea msiba huu kwa imani. 

Prof. Shao alizaliwa mwaka 1944, alisomea shahada ya magonjwa ya vimelea mbalimbali pia amewahi kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978-1981, Mshauri wa wanafunzi UDSM kuanzia 1981-1986, Profesa Mshiriki mwaka 1982-1990, na Profesa tangu 1986. 

Tangu mwaka 1994 alikuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Umoja wa Madaktari Afrika, mwaka 1992, amewahi kuwa mjumbe wa kamati ya mabadiliko ya sekta ya afya Tanzania, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania mwaka 1990-1992. 

Bwana alitoa na Bwana ametwaa Jinala Bwana na Lihimidiwe.